Wednesday, August 12, 2015

YANGA KUIVAA MBEYA CITY JUMAPILI DIMBA LA SOKOINE

Na Gwamaka Mwankota, MBEYA
MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC Jumapili watacheza mechi ya pili katika kambi yao ya Mbeya kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii, Agosti 22, mwaka huu.
Yanga SC watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Sokoine Mbeya Mjini Jumapili, huo ukiwa mchezo wa pili baada ya awali Jumapili kushinda 4-1 dhidi ya Kemondo, Uwanja wa CCM Viwawa, Mbozi.  
Siku hiyo, Yanga SC ilikwenda kupumzika ikiwa nyuma kwa bao 1-0, lakini kipindi cha pili kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm akabadilisha kikosi na timu ikapindua matokeo.
  
Wachezaji wa Yanga wakiwa mazoezini

 
Beki Juma Abdul alimpisha Mbuyu Twite, kiungo Thabani Kamusoko akampisha Said Juma ‘Makapu’, winga Deus Kaseke akampisha Godfrey Mwashiuya na mshambuliaji Malimi Busungu akampisha Amisi Tambwe.
Mwashiuya aliyesajiliwa Yanga SC msimu huu kutoka Kemondo, akafunga mabao mawili, Simon Msuva na Tambwe moja kila mmoja, Yanga ikishangilia ushindi wa 4-1.
Baada ya mchezo huo, Yanga SC ikaenda Tukuyu mkoani Mbeya pia, kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC Agosti 22, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Wapinzani wao, Azam FC wameweka kambi visiwani Zanzibar kujiandaa na mchezo huo- na ikumbukwe mara ya mwisho timu zilikutana katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame wiki mbili zilizopita na Azam FC ikashinda kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 0-0 dakika 90.

No comments:

Post a Comment