WALA huitaji kupiga ramli kutambua Simba
inawaanzisha nani na nani katika mechi ipi. Hii ni kwa mujibu wa mechi
ambazo Wekundu hao wameshacheza hadi leo hii.
Hata kama kocha Dylan Kerr hajaweka
hadharani kikosi chote cha msimu huu, lakini kikosi ambacho
mzungu huyo amekuwa akikipanga kwa ajili ya kutafuta ushindi
kimeshaanza kuonekana.
Katika mechi zote za kirafiki ambazo Simba
ilikuwa inacheza ikiwa katika kambi ya mazoezi ya kisiwani Unguja, kocha
Kerr alikuwa akianza kwa kuwapanga wachezaji kadri alipoona ugumu na
umuhimu wa mechi, lakini katika michezo tafu amekuwa akipanga wachezaji
wa kuamua matokeo ya mechi.
Kerr ambaye msimamo wake ni kuona kila namba inakuwa
na upinzani, alianza kusuka kikosi cha ushindi katika mechi tafu za kirafiki za
kimataifa dhidi ya SC Villa na URA zote za kutoka nchini
Uganda.
Katika mchezo ule wa kirafiki wa kimataifa, Kerr
aliwachezesha wachezaji wake wote aliokuwa nao katika kambi za Lushoto
na kisha Unguja, ambapo katika kila namba kulikuwa na wanandinga wawili
waliocheza katika kiwango sawa na kuwafurahisha wanazi wa klabu hiyo
waliofurika kisawasawa.
Ukiondoa mlinda mlango Vincent Angbang aliyedaka vyema
na kuwa tegemeo, kocha Kerr aliwabadilisha namba wachezaji wengi na
kuthibitisha kinachoitwa kuwa na vikosi viwili katika kikosi cha
msimu huu.
Kikosi cha kwanza kinachoweza kucheza katika ligi ijayo
kinaweza kupangwa kwa langoni kulindwa na Vincent Angban, Hassan
Kessy, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Hassan Isihaka, Juuko Murshud, Justice
Majabvi,Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla, Hamis Kiiza 'Diego', Mussa Hassan Mgosi,
Peter Mwalyanzi.
Katika hiki, Kocha Kerr aliwaanzisha takriban wachezaji wote
hao, isipokuwa Mwinyi Kazimoto aliyeingia baadae na kisha Mwalyanzi
(Peter) alitolewa katika kipindi cha pili.
Kwa upande wa kikosi cha pili, ni dhahiri
langoni atasimama, Manyika Peter 'Junior' Emery Munibona, Samir Haji Nuhu,
Mohamed Faki, Abdi Banda, Jonas Mkude, Issa Ngao, Awadh Juma, Danny
Lyanga, Boniface Maganga na Ibrahim Ajib.
Waliohudhuria mechi ya 'Simba Day dhidi ya SC
Villa watakuwa mashuhuda kuwa, kocha Kerr aliwabadilisha wachezaji wake
kwa mfumo wa kucheza mpira wa kasi na kila mchezaji alipewa jukumu lililofanya
wachezaji wa kikosi kilichopangwa awali na kilichomaliza kuonekana wakiwa
katika viwango sawa kwa spidi ya mchezo, kumiliki mipira na kuwa na
safu ya ulinzi imara.
Akizungumza na mwandishi, Kerr alisema, kwa kiasi
fulani amekamilisha hatua ya kwanza ya kuangalia uwezo wa kila mchezaji
pamoja na mfumo wa kucheza uwanjani.
Alisema, katika hilo, amefanikiwa kuwa na
wachezaji wawili wawili katika kila idara na ndiyo maana kila aliyeingia
kushika nafasi alionekana kumudu vyema majukumu aliyopewa.
"Nilikuwa ninamwangalia kila mchezaji na sasa
nimejiridhisha katika suala la kila namba kuwa na wachezaji wawili wawili.
Nimeridhika na kila mchezaji na kazi iliyopo sasa ni kuendelea kuangalia
suala la nani acheze na nani" alisisitiza Kerr.
No comments:
Post a Comment