Mrithi wa Mavugo apeta Msimbazi
KOCHA wa timu ya soka ya Simba, Dylan Kerr wala hataki kumung'unya maneno kwa Kelvin Ndayisenga kwa kukiri kuwa straika huyo ana mambo mengi yanayompa nafasi ya kufuzu majaribio yatakayomfanya awe miongoni mwa wachezaji watakaosajiliwa msimu huu.
Ndayisenga ambaye ni kama mrithi wa nafasi ya mrundi mwenzie, Laudit Mavugo, alikuwamo katika kikosi cha Simba kilichotoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya URA ya Uganda, katika mechi iliyochezwa Jumamosi iliyopita katika dimba kuu la Taifa, jijini Dar es Salaam.
Straika huyo mwenye umbo la wastani alionesha kiwango cha kuanza kumshawishi kocha Kerr hasa baada ya kuanza kufungua akaunti yake ya mabao akiwa na kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kwa kufunga bao la kuongoza la kipindi cha kwanza.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, kocha wa wekundu hao alisema, straika huyo ana sifa za kuitwa mshambuliaji kwani anatumia vyema mwili na akili zake awapo katika eneo la kufunga, hivyo ameanza vyema majaribio.
Alisema, goli alilofunga dhidi ya URA lilikuwa ni la kutumia akili zaidi kwasababu alikuwa mbele ya mabeki wawili na mlinda mlango na alichokifanya ni ziada ya kutumia vyema utulivu na kuangalia umbali uliopo baina ya mlinda mlango na walinzi wake, ndipo alipofunga bao zuri.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, ana asilimia kubwa ya kupewa nafasi ya kuitumikia Simba, ingawa bado benchi ufundi linaendelea kumfanyia tathimini kabla ya kujiridhisha zaidi katika mazoezi ya kila siku kabla ya kuanza kwa ligi.
"Bado tunaendelea kumwangalia katika mazoezi ya kila siku, lakini katika mchezo wake wa kwanza wa kimataifa dhidi ya URA alicheza katika kiwango cha kuvutia"
"Ameanza vizuri, ni mchezaji anayejiamini kucheza katika nafasi ya ushambuliaji na ameonesha kutambua majukumu yake katika timu kama Simba".
"Ingawa ni mapema kusema lolote juu yake, ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba kama atacheza kwa stahili ya kujituma na kutumia kila nafasi anazopata kwa kufunga ni sawa na kusema kuwa anasimilia kubwa ya kufuzu majaribio". alisema Kerr na kuongeza.
" Nimekuwa nikisisitiza kila siku juu ya utaratibu wangu wa kuanza kumwangalia mchezaji kabla ya kujiaminisha juu ya uwezo na kiwango chake cha uwanjani, hivyo tutaendelea kujiridhisha kwa straika huyo na tutakuwa na majibu katika siku chache zijazo".
Awali, kocha huyo raia wa Uingereza aliuagiza uongozi kuendelea kutupa ndoano za usajili kwa kuzingatia zaidi nafasi ya kupata straika wa kiwango cha juu kwa ajili ya kuongoza safu ya ushambuliaji baada ya kukwama kwa mpango wa Wekundu hao wa kumleta nchini mfumania nyavu Laudit Mavugo.
Iwapo Kelvin Ndeyisenga atasajiliwa, atakuwa ndiye mrithi wa nafasi ya Mavugo ambaye mpango wa kutua katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi ulikwamishwa na klabu yake ya sasa ya Vital'O' kuitaji dau la dola 110,000 ambalo ni sawa na takriban shilingi 220 milioni.
No comments:
Post a Comment