HUU utakuwa mwisho wa ubishi kama anafaa kusajiliwa au
la! Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Simba tayari ameshuhudia kiwango cha
awali cha straika raia wa Senegal, Papa Niang aliyetua jijini
Ijumaa kwa ajili ya majaribio. Lakini amesema kipimo zaidi itakuwa katika
mechi ya dhidi ya timu ya Mwadui.
Timu ya Simba inatarajia kushuka
katika dimba kuu la Taifa, jijini Dar es Salaam, Jumatatu (kesho)
kujipima na timu ya Mwadu inayonolewa na kocha asiyeishiwa maneno,
Jamhuri Khwelo ‘Julio’, hivyo mchezo huo umepangwa kuwa kati ya mtihani
wa majaribio kwa msenegal huyo.
Katika mazoezi ya Jumamosi asubuhi yaliyofanyika katika
uwanja wa Maveterani wa Boko, Kerr alimwangalia Niang katika kila hatua,
kisha akawa anaandika kila jambo katika kitabu chake cha
kumbukumbu, kisha mara kadhaa akiwa anamnong’oneza jambo msaidizi wake Seleman
Matola.
Kerr alisema, atautumia mchezo huo kama kipimo cha awali cha
kuendelea kujiridhisha na kiwango alichonacho msenegal huyo ambaye
ana udugu wa kinasaba na mfumania nyavu tegemeo nchini Senegal, Mamadou
Niang aliyekuja nchini Tanzania kucheza na Taifa Stars na kuisumbua vyema
ngome ya ulinzi.
“Ni mchezaji mwenye jina na hata kiwango
alichokionesha katika mazoezi ya leo asubuhi (jana) ni kikubwa,
lakini bado tunahitaji kuendelea kuona zaidi kazi
yake katika mazoezi yetu yajayo tukiwa kisiwani Zanzibar”.
“Lakini pia tutampa nafasi ya kuonesha kiwango chake
katika mechi ya kirafiki tutatakayocheza Jumatatu (kesho) na timu ya
Mwadui. Huu utakuwa muda mwingine sahihi wa kumwangalia kwasababu tunacheza na
timu ambayo bado siijui ila nasikia wana wachezaji wengi wazoefu wa ligi ya
Tanzania”.
“Wate tutakuwa uwanjani na kila jicho litashuhudia
kiwango cha Niang na baadae tutakuwa naye katika kambi
tutakayokwenda kuiweka kisiwani Unguja, kule tutakuwa naye
kwa siku tano hivi kabla sijatoa jibu la ama asajiliwe au
la!” alisema Kerr na kuongeza.
“Lengo langu ni kupata mchezaji wa nafasi ya ufungaji
atakyeitendea haki idara hiyo, siyo kwa kubahatisha, bali kwa kazi
atakayoionesha uwanjani. Sitaki kufanya usajili wa
kubahatisha, kwani unaweza kuigharimu timu. Ndiyo maana nimetaka kumuona
kila mchezaji kabla ya kupeleka jibu kwa uongozi kama
anastahili kusajiliwa au kuachana naye”
Mshambuliaji Papa Niang, raia wa Senegal
aliyezaliwa Desemba 5, 1988, sasa ana miaka 26 ametua jijini Dar es
Salaam akiwa ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake wa
kuitumikia timu ya CF Mounana ya nchini Gabon ya Magharibi mwa bara
la Afrika.
No comments:
Post a Comment