TIMU ya taifa Tanzania katika soka
la wanawake Twiga Stars, leo alhasiri inajitupa uwanja wa Amaan mjini Zanzibar
kupimana nguvu na wenzao wa Kenya, Harambee Starlets.
Wakenya hao waliowasili juzi asubuhi
katika msafara wa watu 24, wamekuja kwa ajili ya mechi hiyo ya kirafiki ambayo
Twiga Stars wataitumia kama sehenu ya mazoezi kujiandaa na michezo ya Afrika
(All Africa Games) itakayofanyika mwezi ujao nchini Congo Brazaville.
Kikosi hicho kimekuja na wachezaji
17 na viongozi tisa.
Kwa mujibu wa taarifa za Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), pambano hilo linalotarajiwa kuwa la kukata na shoka,
litaanza saa 10:00 jioni.
Wakati walipowasili hapa nchini
juzi, kocha mkuu wa timu hiyo David Ouma, alieleza kuvutiwa na hali ya utulivu,
usalama wa Zanzibar pamoja na ukarimu wa wenyeji.
Hata hivyo, Ouma alisema pamoja na
uhusiano wa miaka mingi kati ya nchi za Tanzania na Kenya, lakini wamekuja
kushinda na hakuna mbadala wa lengo lao hilo.
“Nimekuja na visu vyangu vyote
ambavyo ni vikali na nitavitumia bila huruma kumchinja Twiga keshokutwa (leo)
katika uwanja wa Amaan,” alijigamba kocha huyo.
Amewataja baadhi ya wanasoka wake
tegemeo kuwa ni Merik Nuzia, Tabaka Chacha, Mwanahalima Adam, Huendi Acheni na
Dorias Chitobe.
Sophia Mwasikile ambae ni nahodha wa
Twiga Stars, alisema timu yao iko imara kuwafundisha majirani zao hao jinsi ya
kutumia nafasi za kufunga mabao na kwamba kazi ya kipa wao leo itakuwa kwenda
kuokota mipira nyavuni mfululizo.
Hata hivyo, alitoa indhari kwamba
lengo lao ni kuonesha kiwango kizuri na kwamba mchezo huo sio lengo kubwa kwao,
bali wanachoangalia ni mashindano ya Afrika yaliyo mbele yao.
No comments:
Post a Comment