Thursday, August 6, 2015

BEKI aliyecheza kwa kiwango kizuri akiisaidia Azam FC kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Aggrey Morris hajaitwa kikosi cha awali cha wachezaji 29 wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya kambi ya Uturuki.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa leo ametangaza kikosi cha wachezaji 29 watakaongia kambini siku ya Jumapili tarehe 9, Agosti katika hoteli ya Tansoma iliyopoe eneo la Gerezani kwa ajili ya kambi ya wiki moja ya mazoezi.
Katika kikosi hicho alichokitangaza cha wachezaji 29, Mkwasa amewajumuisha wachezaji watano wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi), ambao baadae watajumuika kwa kambi ya kujiandaa kucheza na Nigeria mwezi Septemba 2015 nchini Uturuki.
  
Aggrey Morris hajaitwa Taifa Stars licha ya kucheza vizuri Kombe la Kagame akiisaidia Azam FC kutwaa ubingwa
 
Taifa Stars inatarajiwa kuweka kambi ya siku kumi jijini Istambul - Uturuki, ambapo itacheza michezo miwili ya kirafiki na timu za Taifa za Libya na Kuwait kabla ya kurejea nchini kuwavaa Nigeria.
Wachezaji watakaongia kambini jumapili ni makipa, Ally Mustafa ‘Barthez’ wa Yanga SC na Aishi Manula wa Azam FC.
Mabeki ni Shomari Kapombe (Azam FC), Michael Aidan (Ruvu Shooting), Juma Abdul, Mwinyi Haji (Yanga SC), Hassan Isihaka (Simba SC), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani (Yanga SC).
Viungo ni Himid Mao, Frank Domayo, Mudathir Yahya (Azam FC), Salum Telela (Yanga SC), Abdi Banda  na Said Ndemla wote wa Simba SC.
Mawinga ni Orgenes Mollel (Aspire – Senegal), Abdrahman Mbambi (Mafunzo), Deus Kaseke, Simon Msuva (Yanga SC), Ramdhani Singano na Farid Mussa (Azam FC), wakati washambuliaji ni John Bocco, Ame Ally (Azam FC) na Rashid Mandawa (Mwadui FC).
Wachezaji wanaocheza nje waliojumuishwa katika kikosi hicho ambacho Agosti 23 kitaelekea kambini nchini Uturuki kwa kambi ya siku kumi ni Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe – DRC), Mrisho Ngassa (Free State - Afrika Kusini) na Hassan Sembi (Santos FC – Afrika Kusini) na Adi Yussuf (Mansfield Town – England).

No comments:

Post a Comment