PAPA Niang |
Nianga ambaye Simba imemrejesha kwao baada ya kushindwa kuonesha makeke aliyotarajiwa kuyafanya katika mechi ya kirafiki kati ya Simba na Mwadui FC ya Shinyanga iliyomalizika kwa sare tasa, amesema kwamba ameshindwa kutamba kutokana na mfumo mgumu wa soka aliloshuhudia.
Amesema kwamba mfumo wa soka la Tanzania ni mgumu sana kwasababu watu wanatumia nguvu nyingi zaidi kuliko maarifa, na wakati mwingine mabeki hawampi mtu hata nafasi ya kudhibiti mpira.
Hata hivyo amekiri kwamba hakuwa kwenye kiwango kizuri kutokana na kukaa nje ya dimba kwa muda mrefu.
Akizungumza na gazeti hili Niang amesema, alikuwa kwenye mapumziko kwa muda mrefu kwahiyo ufiti wake umepungua kwa kiasi kikubwa na tangu amewasili Simba amefanya mazoezi kwa siku mbili na kikosi hicho.
“Nilihitaji nipewe muda zaidi wa kuzoeaa na wachezaji wa Simba, lakini pia kuzoea mfumo wa kocha na aina ya soka analotaka. Kwa bahati mbaya nimeonekana kama sijui mpira, lakini mimi ni straika mwenye heshima kubwa Senegal” amesema.
“Ni kweli sijaonesha kiwango kizuri kwasababu nimetoka likizo, na kila sehemu unapokwenda unahitaji muda ili kuzoea, mimi najaribu kuzoea mpira wa Simba. Sifahamiani na wachezaji, nimefanyanao mazoezi kwa siku mbili na tulikuwa na mechi kwahiyo nilikuwa najaribu kuendana na mfumo wao”, amesema Niang.
Akaongeza: “Kila mahali unapokwenda inabidi ujitahidi kuendana na aina ya soka lao, lakini niliamini kuwa kabla ya ligi kuanza ningekuwa nimezoea mazingira na ningeweza kuonesha ubora wangu”.
Hata hivyo amesema kwamba pamoja na kwamba ametupiwa virago, Simba wangemvumilia wangeweza kupata mambo makubwa kutoka kwake.
“Nilikuja nikiwa na uhakika kwamba kwa rekodi yangu ningesajiliwa. Sijui nini kimetokea, sijui utaratibu ambao unatumika Tanzania. Lakini ngoja watafute mtu mbadala kama wameona kwamba mimi sitawasaidia” amesema.
No comments:
Post a Comment