DYLAN Kerr |
Kerr ameyasema hayo baada ya matokeo ya sare tasa kati ya Simba na Mwadui FC ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, Jumatatu iliyopita.
Akiongea na MWANASOKA, kocha huyo mwenye msimamo mkali amesema kwamba hafurahishwi na safu ya ushambuliaji ya Simba inavyocheza.
“Niwe mkweli, sifurahishwi na mambo yanavyokwenda. Mimi ni kocha ninayetaka matokeo bora. Ninapoitazama safu yangu ya ushambuliaji natamani kusafiri kwenda Ulaya kusaka washambuliaji” amesema kocha huyo.
Alipoulizwa kwamba haoni kama washambuliaji wa Ulaya ni ghali sana kucheza Tanzania, alishangaa na kusema:
“Nani kakwambia kuna watu ghali Ulaya? Mimi nafahamu kuna watu watu wanaweza kuja kucheza hapa kwa mshahara huo huo wanaolipwa Waafrika. Tatizo muda wa kufanya hivyo kwasasa sina, Ligi inakaribia kuanza na usajili ndio huu mnaouona matokeo yake”.
Amesema kwamba katika bara la Ulaya na hata Amerika ya Kusini kuna baadhi ya wachezaji wazuri sana ambao hawapati nafasi katika nchi zao, na wangependa kucheza ili kulinda vipaji vyao na kuishi.
Ametoa mfano wa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Andrey Countinho akisema kwamba katika nchi anakotoka ya Brazil kuna wachezaji wa maana sana ambao hawana nafasi kutoka na ushindani mkubwa wa soka la taifa hilo.
“Katika nchi kama Brazil anakotoka yule mchezaji wa Yanga, katika nchi kama Mexico na Uruguay kuna wachezaji ambao ukiwaleta hapa ni lulu kubwa” amesema.
Kocha huyo amesema jambo moja alilogundua ni kwamba wachezaji wengi wa Afrika hawajitumi ipasavyo, lakini akasema kwamba kama kocha anayafanyia kazi matatizo yaliyojitokeza katika kikosi chake kwa sasa.
Kauli hii ya Kerr inaleta tafsiri kwamba ikiwa wachezaji wa Simba hawataongeza bidii, kocha huyo anaweza kutumia nafasi ya usajili katika dirisha dogo kusajili wachezaji kutoka Ulaya wanaoweza kuisaidia Simba.
No comments:
Post a Comment