WEKUNDU wa Msimbazi, timu ya soka ya Simba wako katika mazoezi ya mwisho kabla ya kuingia katika mbio za kuwania Ubingwa wa Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara.
Simba wameweka kambi katika mji ambao wana bahati nao wa Zanzibar, na mazoezi yanayoendelea hapa tangu wametua juzi, ni sawa mgonjwa anayepewa dozi kutwa mara mbili.
Na kama kawaida yao, Wekundu hao wamekuwa wakifanya mazoezi hayo katika uwanja wa Amaan, muda wa asubuhi na jioni.
Kocha msaidizi wa Simba Suleiman Matola amesema mazoezi yanakwenda vizuri, na wataitumia michezo ya wikiendi hii ya kirafiki kama kipimo cha kuwanoa na kuwatazama wachezaji wake kwa mara nyingine.
“Tumeanza mazoezi vizuri tunatarajia kukaa hapa mpaka tarehe 9 ya mwezi ujao, pengine siku hiyo tutarejea bara tayari kucheza ligi kuu”, alisema Matola.
Kuhusu wachezaji wawili wa kigeni ambao simba wanatarajia kumchagua mmoja atakae wafaaa Matola amesema mmoja ameshafika visiwani na mmoja alitarajiwa kufika wakati wowote. Wachezaji ambao ni Pape na Ndembele, mmoja raia wa Mali na mwengine ni Msenegal.
“Ndio maana tunacheza michezo miwili ya kirafiki, dhidi ya JKU na Mafunzo ambao ndio mabingwa wa ligi kuu soka Zanzibar ili tuweze kuchagua mmoja anayetufaa”, amesema Matola.
Hata hivyo Simba inawakosa baadhi ya wachezaji wake muhimu walioko katika timu ya taifa ya Tanzania pamoja na ile ya Uganda.
Beki wake katili, Juuko Murshid hayuko katika kikosi kilichoko Zanzibar kwasababu ameitwa kwenye timu ya taifa ya Uganda, “The Cranes”. Walioko katika timu ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars” ambayo imepiga kambi nchini Uturuki ni mabeki Hassan Isihaka, Mohammed Hussein “Tshabalala”, viungo Abdi Hassan Banda na Saidi Ndemla pamoja na mshambuliaji Ibrahim Ajibu.
No comments:
Post a Comment