Thursday, August 27, 2015

Simba yampata mrithi wa Mafisango


UKILITAJA jina la Patrick Mafisango katikati ya wanachama na washabiki wa klabu ya soka ya Simba, lazima watamkumbuka kwa simanzi! Kisha watakwambia 'Achana na ile Mashine, ni kiraka'.

Ukiwauliza sababu ya kuitwa 'kiraka' watakujibu, alikuwa na sifa ya kucheza kama, mlinzi, kiungo mkabaji na hata straika, wa kutuminiwa.

Huyu ndiye Mafisango (Patrick) ambaye amefariki dunia Mei 17 mwaka 2012 kwa ajali ya gari katika eneo la VETA, Chang'ombe, jijini Dar es Salaam, akiacha pengo kubwa la sifa ya mchango wale katika kikosi cha Msimbazi.

Lakini, kama ulikuwa katika mechi ya Simba dhidi ya Mwadui, kuna mchezaji mmoja anaitwa Justice Machabvi, huyu bwana achana naye, aliweka historia ya kucheza katika namba tatu tofauti dimbani kiasi cha kumshangaza Kocha Dylan Kerr na kulazimika kumvulia kofia na kumwita 'kiraka'.

Katika mechi ile iliyopigwa katika dimba la Taifa, Jumatatu iliyopita na Simba kutoshana nguvu na Mwadui kwa Suluhu, Machabvi, raia wa Zimbabwe alikuwa katika kiwango cha juu kiasi cha kumfanya Kerr azungumze ya mayoni.

Machabvi ambaye amesajiliwa kwa kandarasi ya miaka miwili, alianzishwa katika kikosi cha kwanza katika nafasi ya kiungo mkabaji na kuimarisha vyema ulinzi wa kikosi cha Wekundu hao.

Lakini, wakati ambapo timu ilipoendelea kupambana kwa ajili ya ushindi, Machabvi mara moja aliambiwa acheze kama kiungo wa kupandisha mashambulizi, kazi aliyoifanya na kumkuna kocha mzungu.

Wakati ambapo kocha Dylan Kerr alipobadilisha kikosi takriban kwa asilimia themanini, Justice Machabvi alipangwa kucheza katika nafasi ya ulinzi wa katikati, hasa baada ya kutolewa kwa 'mkoba' wa kutumainiwa, Juuko Murshid.

Katika kipindi hicho cha pili, Machabvi alionekana kumudu vyema nafasi ya beki wa kati kiasi cha kumfurahisha Dylan Kerr ambaye mara baada ya mchezo alimwagia sifa mzimbabwe huyo kwa kumwita 'kiraka'.

Kerr alimzungumzia Machabvi kama aina ya wachezaji anaotaka kuwa nao katika kikosi cha msimu huu kwa sababu wanabebwa na sifa ya kucheza katika namba zaidi ya tatu uwanjani.

"Machabvi ni aina ya wachezaji ninaowataka, alicheza vizuri na hata kuziba mapengo yaliyojitokeza wakati mchezo unaendelea".

"Ninahitaji wachezaji kama huyu, anayeweza kupewa jukumu na kulitekeleza vyema. Katika soka la zama hizi mchezaji lazima awe na uwezo wa kucheza zaidi ya namba mbili ama tatu". alisema Kerr.

Awali mara baada ya kutua kwa ajili ya kuinoa timu ya Simba, Kerr aliuambia uongozi azma yake ya kutaka kusajiliwa wachezaji walio na uwezo wa kucheza zaidi ya namba mbili dimbani.

No comments:

Post a Comment