Thursday, August 27, 2015
Funga kazi
WAKATI dirisha la usajili linafungwa rasmi Jumatatu ijayo, Simba imelazima kufunga usajili huo kwa kishindo.
Katika hatua unayoweza kuita ni “Funga Kazi”, Simba imelazimika kutumia tena fedha kumtumia tiketi ya ndege, straika wa kimataifa wa Senegal Pape Abdoulaye N'Daw mwenye umri wa miaka 21 ambaye amekuja kuchukua nafasi ya Msenegali mwenzake Papa Niang ambaye alichemsha katika majaribio.
N’Daw hadi mapema wiki hii alikuwa anacheza katika timu ya Dinamo Bucuresti ya nchini Romania, lakini Simba haikulitazama hilo, ikamvuta kuja Msimbazi.
Kiongozi mmoja wa wekundu hao wa Msimbazi ameliambia MWANASOKA kwamba Simba imeachana na Msenegali, Papa Niang baada ya kumjaribu kwa dakika 45 tu jana katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Huu sasa ni usajili wa mwisho, tuna hakika kabisa kwamba Simba tutapata straika ambaye kocha wetu anamtaka. Shida sio kuwa na mshambuliaji tu, lakini kuwa na mshambuliaji ambaye ni wa kimataifa mwenye uwezo wa maana sana” amesema kiongozi huyo.
Licha ya Pape Abdoulaye N'Daw kinda mwenye umri wa miaka 21, Simba pia ilikuwa katika mikakati ya mwisho kumpata mshambuliaji mwingine wa kimataifa kutoka Mali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amekaririwa akisema Msenegali huyo na mchezaji mwingine kutoka Mali watafanyiwa majaribio na atakayevutia zaidi, ndiye atapewa mkataba.
Niang alikuja SImba SC baada ya klabu hiyo kushindwa kufikia makubaliano na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Kevin Ndayisenga juu ya dau la usajili.
Niang kutoka klabu ya Alianza F.C. ya El Salvador ambaye ni mdogo wa mshambuliaji wa kimataifa wa zamani wa Senegal, Mamadou Niang jana alishindwa kabisa kuwashawishi wana Simba kwa soka yake.
Mchezaji huyo wa zamani wa CF Mounana ya Gabon, Al Shabab SC ya Kuwait, FC Vostok ya Kazakhstan, FF Jaro, AC Oulu na FC OPA za Finland alitarajiwa kuondoka kurejea kwao, ikiwa ni baada ya siku tatu za kuwa Dar es Salaam.
Awali Simba SC pi ilishindwa kumsajili mshambuliaji mwingine hatari wa Vital’O, Laudit Mavugo kufuatia klabu mbili za nchini humo kupandisha thamani ya mchezaji huyo na kuwa Sh. Milioni 200, badala 110 walizokubaliana awali.
Aidha, kuibuka pia kwa mzozo mpya kati ya klabu ya Vital’O FC na Solidarity FC, inayodai kumlea Mavugo na kudai ina hakimiliki ya mchezaji huyo nako kuliishitua Simba. Vital’O ikaikoroga zaidi Simba SC baada ya kudai kiwepo kipengele cha wao kupata asilimia 50 kama mchezaji huyo atauzwa na Wekundu hao wa Msimbazi kwenda klabu nyingine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment