Thursday, August 27, 2015

Julio aisifu Simba, lakini ajitabiria ubingwa


JAMHURI Kihwelo
KOCHA wa Mwadui FC Jamhuri Kihwelo amesema kwamba Simba ni timu nzuri, lakini akasema kwamba Mwadui ndiyo wataibuka mabingwa wa ligi kuu msimu ujao.

Kocha huyo ambaye aliwahi pia kuwa kocha wa Simba amesema kwamba jeuri hiyo inatokana na usajili, maandalizi na marekebisho madogo atakayoyafanya kwenye kikosi chake baada ya kubaini makosa machache kwenye kikosi hicho.

Julio alizungumza mara baada ya kumalizika kwa mechi ya kirafiki ya kujipima nguvu kati ya Mwadui FC dhidi ya Simba SC kuelekea michuano ya ligi kuu Tanzania bara itakayoanza Septemba 12 mwaka huu.

“Kwanza nashukuru Mungu kucheza mechi ambayo ni kipimo kizuri kwangu maana nimeshacheza mechi na timu za Ligi Kuu takribani sita sasa na nimeona kadiri siku zinavyozidi kwenda wachezaji wangu wanabadilika ingawa leo nimecheza nikiwa na wachezaji saba wakiwa wako majeruruhi. Chuji anaumwa, Mnyati anaumwa, Antony Matogolo na wengine wengi”.

“Kwangu hiyo siyo ishu kwa maana nimesajili wachezaji kwa ajili ya Ligi kuu lakini uwezo wa ya timu yangu nimeifurahia kwa jinsi walivyocheza ingawa hatukupata goli”.

“Simba ni timu nzuri ila wao walichokosea ni kutudharau sisi na kuona sisi hatuna uwezo na wao kujiona timu yao inauwezo kuliko sisi. Hata kabla hatujacheza kuna baadhi ya wachezaji walisema, sisi tuna vijana wanapenya mtafungwa goli tano. Mimi nikawaambia uwezo wa kutufunga goli tano hamna twendeni tukacheze mpira”.

Julio akaendelea kwamba “Kingine naujua vizuri huu uwanja, walivyokuja walicheza kwa nguvu kwa presha ili kupata goli za mapema kwahiyo kadiri muda ulivyokuwa unakwenda halafu goli hawapati, morali ikawa imeshuka timu yangu ikatulia na kucheza vizuri ingawa hatukupata goli lakini performance mimi nimeifurahia hususan safu ya ulinzi na viungo wamecheza vizuri sana”.

Kocha huyo akasema tena “Mimi ndio nakuwa bingwa mwaka huu, nikisema hivyo watu wanacheka na kuniona mimi mwendawazimu. Lakini si mnajua kwamba sisi sote tutakufa? Lakini hatujui tutakufa lini kwahiyo kama wenzetu wametangulia wamekufa na sisi tutakufa kwahiyo hata mimi timu yangu inaweza kuwa bingwa. Tupo katika mashindano, basi nitajieni nyinyi timu itakayokuwa bingwa kwenye msimu huu tunaotarajia kuuanza mwezi Septemba”. “Kila timu ambayo imesajili, imejipanga, malengo yake ni kushinda kwahiyo na sisi tutapambana kwenye mbio ndefu halafu baadae ndio bingwa atapatikana lakini kwa timu yangu nilivyoiandaa na makosa ambayo nimeyaona nikiyafanyia marekebisho, kwa nini nisiwe bingwa?”.

No comments:

Post a Comment