Thursday, August 20, 2015


Kerr: Nisilaumiwe kuhusu Maguri

ELIAS Maguri

KOCHA Mkuu wa Simba, mwingereza Dylan Kerr amesema kwamba hapaswi kulaumiwa kwasababu ya kumwondoa katika kikosi hicho straika Elias Maguri.

Akizungumza na MWANASOKA, kocha huyo amesema kwamba Maguri aliomba yeye mwenyewe kuondoka Simba baada ya kugundua kwamba hana nafasi katika kikosi cha kwanza.

“Ni yeye mwenyewe aliomba kuondoka baada ya kuona nafasi yake katika kikosi cha kwanza ni kama haipo. Niliwataarifu viongozi na kuwaambia kwamba huyu bado ni kijana mdogo, wamtafutie timu akakuze kipaji kwa mkopo. Sikumwondoa kabisa, sina mamlaka hiyo” amesema Kerr.

Amesema alichofanya ni kumshauri, na yeye mwenyewe akawa amekubali.

Hata hivyo, anasema anashangazwa na kauli za washabiki wa soka wanaodai kwamba wamemkariri Maguri akilalamika.

“Kama ni kweli atakuwa analalamika atakuwa anafanya makosa. Yeye alitakiwa kutazama maisha yake ya soka. Kama unakaa katika timu huna nafasi ya kucheza, unaomba kutolewa kwa mkopo ukacheze ili mpira wako usife. Kama hilo limekamilika, unataka kuachwa moja kwa moja unalalamika nini?” amehoji Kerr.
  
Amesema kwamba yeye anachofahamu ni kwamba viongozi walimwambia kwamba  mchezaji huyo ana mkataba, na yeye kocha awaambia kwamba basi wamtafutie timu akaongeze uwezo.

“Kama leo yanazungumzwa maneno kwamba kocha nimemkataa mchezaji sio sahihi. Mimi nataka kuona kila mchezaji aliyesajiliwa Simba anaonesha uwezo wake kwa manufaa ya Simba” alisema.

No comments:

Post a Comment