Wednesday, August 12, 2015

PEDRO: BENCHI LINAKIMBIZA BARCELONA

WINGA wa Barcelona, Pedro amethibitisha ataondoka klabu hiyo kuhamia Manchester United baada ya kuwa shujaa wa mechi ya Super Cup iliyodumu kwa dakika 120 jana usiku Georgia.
Baada ya kufunga bao la ushindi dakika za lala salama, Barca ikishinda 5-4 dhidi ya Sevilla, Pedro alisema; "Ni mazingira magumu kwangu. Sitaki kuondoka, lakini ni suala la muda (mchache) wa kucheza, imeendelea kuwa hivi kwenye timu kwa miaka michache sasa,".
Hayo na kuonekana akiwa mbali na wenzake wakati wanasherehekea taji la Super Cup Uwanja wa Dinamo Arena yanathibitisha kauli za Mkurugenzi wa Barcelona, Robert Fernandez kwamba aliiambia klabu anataka kuondoka.
Manchester United iko tayari kutoa Pauni Milioni 22 kumnunua Pedro

Rais wa Barcelona, Josep Bartomeu amerudia kusema jana kwamba hataki mchezaji huyo aondoke. Lakini uamuzi ulikwishafanyika tangu msimu uliopita wakati Pedro alipokumbushia amekaribia mwisho wake katika klabu hiyo.
Na ndiyo maana dau lake limeshuka kutoka Euro Milioni 150 hadi Milioni, sawa na Pauni Milioni 22 huku pande zote zikiwa zimefikia makubaliano juu ya hilo.
Kilichobaki sasa kuamua safari yake ya Manchester na kauli ya kocha Luis Enrique ambaye alisema anataka mchezaji huyo awepo katika mechi zote za Super Cup ya Ulaya na Hispania itakayochezwa Ijumaa na Jumatatu Bilbao na Nou Camp.
Lakini uamuzi wa kumuweka benchi jana katika mechi na Sevilla unazidi kuongeza uwezekano wa kuondoka.

No comments:

Post a Comment