Sunday, August 30, 2015
Murshid ampagawisha Micho
KOCHA mkuu wa timu ya taifa ya Uganda “The Cranes”, Milutin 'Micho' Sredojević amesema kiwango cha beki wa kati wa Simba, Juuko Murshid ni kikubwa mno.
Kocha huyo raia wa Serbia aliyewahi kuinoa Yanga ya Tanzania, amesema kwamba kiwango cha beki huyo wa Simba kimekuwa kikiongezeka kila siku, na akakiri kwamba anaweza kuwa beki bora katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
“Namjua Juuko, naona kila siku kasi yake inaongezeka. Anaonekana kuna mambo ameongeza sana katika soka lake ndio maana nimelazimika kumwita katika timu ya taifa” amesema Micho.
Ameisifu Simba kwa kumwongezea makali beki huyo akisema kwamba kila anaporejea Uganda anakuwa na vitu vipya kabisa.
“Ingawaje watu wengi wanasema kwamba ndiye beki katili na mtukutu zaidi katika Uganda na Afrika Mashariki pia, lakini kwangu mimi naona kwamba hiyo ndiyo staili yake ya kuzuia washambuliaji wakali”, amesema kisha akaongeza;
“Hata hivyo huwa namwambia kwamba anapocheza mpira lazima ahakikishe kwamba rafu zake hazileti madhara kwa timu. Nadhani hata huko Simba, rafu zake hazijaigharimu kabisa timu, vinginevyo asingekuwa chaguo la kwanza la mwalimu” amesema.
Kocha huyo amesema kwamba siku zote mwalimu makini humtazama na kumpenda beki ambaye anaogopewa na washambuliaji wakorofi pia.
“Kwangu mimi nampenda Murshid kwa staili yake ya kuwadhibiti washambuliaji wanaoitwa wakorofi. Hii ndiyo beki ya kazi” alitamba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment