MCHEZAJI WA YANGA ATUA KUKIPIGA DARAJA LA KWANZA
Klabu ya Ruvu Shooting leo
imefanikiwa kumsajili aliyekuwa kiungo wa Yanga Hassan Dilunga mara
baada ya mchezaji huyo kuvunja mkataba na wanajangwani kufuatia
kushindwa kuelewana kati ya pande hizo mbili hatimaye mchezaji huyo kuwa
huru.
Afisa habari wa Ruvu Shooting
Masau Bwire amethibitisha Dilunga kusajiliwa na Ruvu Shooting ambayo
msimu ujao itashiriki ligi daraja la kwanza baada ya kushuka daraja
kwenye mechi yake ya mwisho ya ligi kuu msimu uliopita (2014-2015)
ilipocheza dhidi ya Stand United na kupoteza mchezo ambapo moja kwa moja
ikashuka daraja.
Awali klabu ya Yanga ilitoa
taarifa ya kumpeleka Dilunga kwa mkopo kwenye klabu ya Stand United
lakini inasemekana mpango huo ulishindikana kutokana na mchezaji huyo
kutofikia makubaliano na klabu ya Stand United, hatimaye kujiunga na
maafande hao wa JKT kutoka mkoani Pwani.
Lakini mpaka sasa bado
haijafahamika kuwa Dilunga amejiunga na klabu hiyo kwa mkataba wa muda
gani. Pindi taarifa hiyo itakapokuwa tayari, mtandao huu utakujuza.
No comments:
Post a Comment