Sunday, August 30, 2015
Kimwaga: Nitaonesha makali Simba
KIUNGO mpya wa Simba, Joseph Kimwaga amekiri wazi kuwa alikata tamaa ya kucheza mpira baada ya mambo kuwa magumu katika klabu ya Azam FC, lakini sasa ataonesha makali yake.
Kimwaga licha ya kushindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Azam FC alisumbuliwa na majeraha ya goti kiasi cha kufanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini.
Mchezaji huyo anayetumia mguu wa kushoto anakumbukwa na wapenzi wengi wa mpira nchini kutokana na kufunga goli la ushindi katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga SC Novemba, 2013 wakati Azam iliposhinda 3-2.
“Baada ya kuumia na kuwa nje kwa muda mrefu nilianza kukata tamaa kama kweli ningeweza kurudi katika kiwango changu cha kawaida. Kusajiliwa na Simba nitachukulia kama njia ya kurejesha makali yangu” anasema Kimwaga kwa njia ya simu akiwa kambini Zanzibar.
Simba imekuwa Zanzibar kwa kambi ya mwisho kabla ya kuanza kwa ligi kuu Septemba 12, itacheza na JKU ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki siku ya Jumapili hii.
Kimwaga tayari amecheza gemu moja ya maandalizi wakati timu hiyo ilipotoka sare ya bila kufungana na Mwadui FC wiki iliyopita anatajwa kama mtu wa kuchukua nafasi iliyoachwa na winga Ramadhani Singano ‘Messi’ ambaye amejiunga na Azam FC.
“Nipo hapa kufanya kazi, lengo langu ni kushirikiana na wenzangu kuisaidia Simba msimu huu. Najifua ili kumshawishi mwalimu nipate nafasi ya kucheza mara kwa mara. Unajua nimekuwa nje ya uwanja kwa mwaka mzima kutokana na majeraha. Anasema Kimwaga ambaye tangu amepona hakuwahi kuichezea Azam FC katika mechi ya ushindani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment