HAKUNA kulala hata kidogo Msimbazi! Simba imeamua kufanya kweli tena kwa kusaka mfumania nyavu ambapo jana imeshusha mtambo wa mabao kutoka nchini Mali.Huyu ni Makan Dembele.
Straika huyu mwenye umbile la maana amewasili nchini kwa majaribio chini ya kocha Dylan Kerr.
Kwa mujibu wa takwimu, Dembele ametua nchini akitokea katika klabu ya JS Kabylie ya Algeria.
Taarifa za ujio wa mpachika mabao huyo zinasema kuwa, mara baada ya kutua jijini Dembele anatarajia kuungana na kikosi cha Simba kinachokwenda kuweka kambi ya mazoezi kisiwani Unguja.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Wekundu hao, Zacharia Hans Poppe alithibitisha kutua kwa mchezaji huyo na kwamba ni kati ya wachezaji wawili wanaokuja kufanya majaribio ya kuitumikia Simba ya msimu ujao wa ligi.
Hans Poppe alisema,awali kabla ya kuja nchini kamati yake ilikuwa na mawasiliano na wakala mbalimbali wa nchi za Afrika Magharibi na ndiyo waliosaidia kupatikana kwa Dembele na msenegal Pape Abdoulaye N'Daw aliyewasili kwa ajili ya majaribio.
"Ni kweli tumempokea Dembele na N'Daw ambao wamekuja kwa ajili ya majaribio kabla ya kufanyika kwa hatua nyingine za kiufundi na usajili utakaozingatia matakwa na maelezo ya benchi la ufundi". "Kocha Dylan Kerr ndiye aliyeachiwa jukumu la kuwaangaalia kiufundi kabla ya kutoa majibu ya mwisho ya kama wamefuzu au la" alisema Hans Poppe.
No comments:
Post a Comment