TFF lawamani kuigwaya Yanga
SEIFEDDIN Jamal |
MWANACHAMA wa klabu ya soka ya Simba, Seifeddin Jamali marufu kama 'Sefu Simba' amelitupia lawama Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF) kwa kulifumbia macho suala la uchaguzi wa klabu ya soka ya Yanga ambayo mpaka sasa haijafanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya shirikisho hilo.
Awali, klabu ya soka ya Yanga ilitakiwa kufanya uchaguzi mkuu mapema jana, lakini wakasikika kusogeza mbele hadi mwaka huu, lakini hata hivyo hajafanya hadi sasa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Jamali alisema, kitendo cha Yanga kutofanya uchaguzi ili hali TFF ikibaki kimya haileti usawa wa kikatiba na kanuni ya shirikisho hilo.
Alisema, inashangaza kuona TFF imekuwa wakali kwa kuzitaka baadhi ya klabu kufanya uchaguzi, lakini imeshindwa kuonesha ukali huo kwa Yanga na kuiacha ijiamulie muda wa kufanya uchaguzi huku shirikisho likiwa kimya.
Jamali ambaye amewahi kuwa Mtunza Hazina wa klabu ya soka ya Simba katika miaka ya Themanini anakumbuka namna TFF ilipoishupalia Simba kufanya uchaguzi ili hali haioneshi nguvu hizo kwa klabu ya soka ya Yanga.
"TFF walionesha nguvu nyingi katika kuitaka klabu ya soka ya Simba kufanya uchaguzi, lakini inashangaza kuona ipo kimya katika suala la kuitaka Yanga kufanya uchaguzi, hii naona haijakaa sawa hata kidogo".
"Hata ukiangalia hivi sasa, takriban klabu na timu zote za Ligi Kuu tayari zimefanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya TFF, lakini kwa upande wa Yanga bado hawajafanya na shirikisho linaonekana kukaa kimya, hii maana yake nini?" alihoji Jamali na kuongeza.
"Lazima shirikisho lioneshe usawa katika kila hatua ya kusimamia kanuni zake kama msimamizi wa soka la Tanzania, lakini kinachooneka hivi sasa ni kama wanaigwaya Yanga".
Kauli ya Jamali inakuja siku chache ambapo timu mbalimbali za Ligi Kuu tayari zimekamilisha zoezi la uchaguzi, zikiwemo Coastal Union na African Sports ambazo zimeshachagua viongozi wao kwa mujibu wa katiba zao na ile ya TFF.
Katika hatua nyingine Jamali ameupongeza uongozi wa Simba kwa kuendesha vyema wiki ya Simba ambayo hitimisho lake ndiyo inayoitwa 'Simba Day' na kusema hatua hiyo inaendeleza umoja ndani ya klabu.
Alisema, Simba Day ya mwaka huu ilifana sana na kuwafanya wanachama na washabiki wa klabu hiyo kuwa kitu kimoja, hatua ambayo imeongeza mshikamano kwa wanasimba popote walipo.
" Simba Day ni siku muhimu kwa wanasimba kuongeza mshikamano wao ambao ni muhimu kwa timu kufanya vizuri, hivyo naendelea kuwapongeza viongozi na kuwataka kuendelea kuhimiza umoja ndani ya klabu ambao ni nguzo muhimu ya ushindi wa timu" alisema Jamali.
No comments:
Post a Comment