Saturday, August 8, 2015

BONGE LA KIPA LA BRAZIL KUTUA SIMBA KESHO



KIPA Mreno mwenye asili ya Brazil, Ricardo Ribeiro de Andrade (pichani) anatarajiwa kutua kesho Dar es Salaam kwa ajili ya kujiunga na Simba SC.
Kaimu Katibu Mkuu wa Simba SC, Collin Frisch amesema kwamba, mlinda mlango huyo mkongwe wa umri wa miaka 39 atawasili pamoja na mshambuliaji kutoka Mali, Makan Dembele.
Dembele anayetokea JS Kabylie ya Algeria na kipa huyo anayesifika kwa kuokoa hadi michomo ya penalti, watawasili Alfajiri ya kesho.
Aidha, Simba SC leo imempokea mshambuliaji wa Atletico Sport Olympic ya Burundi, Kevin Ndayisenga anayekuja kwa ajili ya majaribio.
Ndayisenga ameletwa ili kuangalia uwezekano wa kuziba pengo la mshambuliaji wa Vital’O ya Burundi pia, Laudit Mavugo, aliyetakiwa na klabu hiyo awali.
Simba SC iliamua kuachana na Mavugo baada ya klabu mbili za nchini humo kupandisha thamani ya mchezaji huyo na kuwa Sh. Milioni 200, badala 110 zilizokubaliwa awali.
Aidha, kuibuka pia kwa mzozo mpya kati ya klabu ya Vital’O FC na Solidarity FC, inayodai kumlea Mavugo, hivyo nayo kudai ina hakimiliki ya mchezaji huyo nako kuliishitua Simba.
Vital’O ikaikoroga zaidi Simba SC baada ya kudai kiwepo kipengele cha wao kupata asilimia 50 kama mchezaji huyo atauzwa na Wekundu hao wa Msimbazi kwenda klabu nyingine.
Mshambuliaji Makan Dembele anatarajiwa kuwasili kesho Simba SC

Pamoja na hayo, Simba SC ilifanikiwa kusajili mchezaji mwingine wa Vital’O, beki wa kushoto na kulia, Emery Nimubona ambaye tayari yupo nchini.
Tayari Simba SC inaye kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast aliyekuja kwa majaribio ambaye amekwishaidakia timu hiyo mechi tatu na kufungwa mabao mawili tu katika mchezo dhidi ya KMKM, Wekundu hao wa Msimbazi wakishinda 3-2. 
Na wakati bado kocha Muingereza, Dylan Kerr hajaamua kuhusu kipa wa zamani wa timu ya vijana ya Chelsea chini ya umri wa miaka 21, Angabn- anakuja Ricardo Ribeiro de Andrade.

No comments:

Post a Comment