Sunday, August 23, 2015

Stars bila Kazimoto, wadau wapigwa butwaa


MWINYI Kazimoto

KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ametaja wachezaji 22 watakaosafiri leo usiku kuelekea nchini Uturuki kwa kambi ya mazoezi bila jina la kiungo mwenye uwezo mkubwa kwasasa hapa nchini Mwinyi Kazimoto wa Simba.

Kazimoto anayejua kubadili hali ya mchezo kutokana na soka lake maridadi, hatakuwepo katika kambi ya Uturuki ya wiki moja ni maalum kwa ajilu ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria Septemba 05, 2015.

Orodha  ya wachezaji 22 imetoka katika kikosi kilichotangazwa wiki mbili zilizopita na kocha mkuu wa Taifa Stars, ambapo walipata nafasi ya kufanya mazoezi kwa takribani wiki moja katika uwanja wa Karume.

Wachezaji waliochaguliwa ni Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga SC), Aishi Manula (Azam FC), Said Mohamed (Mtibwa Sugar), walinzi Shomari Kapombe (Azam FC), Abdi Banda, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka (Simba SC), Juma Abdul, Haji Mngwali, Kelvin Yondani, Nadir Haroub (Yanga SC).

Viungo Mudathir Yahya, Himid Mao, Frank Domayo (Azam FC), Salum Telela, Deus Kaseke (Yanga SC), Said Ndemla (Simba SC), Washambuliaji John Bocco, Farid Mussa, (Azam FC), Rashid Mandawa (Mwadui FC), Simon Msuva (Yanga SC), na Ibrahim Hajib (Simba SC).

Taifa Stars inatarajiwa kuondoka  usiku wa Jumapili hii kwa usafiri wa shirika la ndege la Uturuki (Turkish Airlines), na kufika Jumatatu asubuhi jijini Istambul, ambapo timu itaelekea katika mji wa Kocael ambapo itaweka kambi ya wiki moja katika hoteli ya Green Park Kartepe.

 Baadhi ya wa washabiki wa soka hapa nchini wamesema kwamba Mkwasa hajaitendea haki nafasi ya kiungo kwa kumuweka nje kiungo fundi na mwenye uzoefu mkubwa wa kimataifa, Kazimoto.

Wadau hao wa mpira wamesema kwamba Kazimoto ni mzuri sana na kwamba angeshirikiana na Salum Telela na Saidi Ndemla pamoja na Frank Dumayo, Stars ingekuwa na matokeo mazuri zaidi.

No comments:

Post a Comment