Sunday, August 23, 2015

Simba yasajili straika dakika za lala salama


ACHANA na  huyu straika Papa  Amodou Niang raia wa Senegal ambaye  tayari ametua  jijini na ameshaanza  kufanya majaribio yatakayotoa majibu   ya ama apewe kandarasi au la, kuna   taarifa mpya kuwa,  Wekundu hao  wanamleta mpachika mabao mwingine  wa kuja kupiga mzigo.

Taarifa za uhakika zilizonaswa na mwandishi wa  habari  hizi zinasema kuwa, dili la kumleta   straika  hilo lipo mikononi mwa  wakala wa nchini Cameroon ambaye anakamilisha  taratibu za mwisho za kumwezesha mwanandinga  huyo kutua  jijini  siku  yoyote kuanza jumatatu.

Ingawa  taarifa  hizo bado ni siri, lakini Mwanasoka linatambua kuwa, straika huyo ana umri wa miaka 24 na ni raia wa Cameroon, lakini  hata  hivyo jina  halisi na   klabu anayotoka linafanywa kuwa  siri hadi  kila kitu kitakapokamilika.

Imeelezwa zaidi kuwa,  awali  ujio   wa mpachika nyavu huyo ulipangwa kufanyika kabla ya jumatano iliyopita, lakini kulikuwa na tatizo la kukamilika kwa hati ya kusafiria mchezaji  huyo ambayo ilitakiwa kubadilishwa kwasababu  awali alikuwa anatumia viza ya nchini 

Uturuki anakocheza  soka la kulipwa katika  klabu hiyo ya daraja la pili.
Chanzo chetu makini kilicho na kila  data za mwanandinga  huyo  kinasema kuwa, ujio wa  mcameroon huyo ni harakati za Kamati ya Usajili  ya Wekundu hao inayotaka kutimiza kazi  waliyopewa na kocha Dylan Kerr anayetaka kuona Simba inafunga usajili ikiwa na straika  mkali wa kufumania nyavu.

Kerr ambaye  mpaka sasa ameridhika na wachezaji aliona nao,  amekuwa akisisitiza kuwa  bado kikosi chake kinahitaji  straika  mwenye kazi moja tu ya kutupia mpira kambani na kuipa ushindi  timu katika kila mchezo.

Katika  hatua hiyo, kuja kwa  mcameroon  huyo kumetajwa kama  mmoja ya wachezaji ambao wataufunga msimu wa  usajili wa  Simba iwapo atajaribiwa na kukidhi  vigezo anavyovitaka kocha Dylan Kerr.

Taarifa za  ujio wa straika  huyo zinakuja  huku  mfumania nyavu  Kelvin Ndayisenga  aliyekuja kufanya majaribio ndani ya kikosi cha Wekundu hao akirejea kwao nchini Burundi  baada ya Simba kutokuwa  tayari kulipa lundo la  mafungu ya usajili  wa mchezaji   huyo ililifikia kiasi cha dola  za kimarekani 70,000 ambazo ni sawa na hela za madafu 140,milioni.

Mlolongo  huo ambao Simba waliamua kuachana nao ni pamoja na kutakiwa kuilipa klabu yake ya Vital’O’, wakala na fedha zake Ndayisenga mwenyewe, kiasi ambacho Wekundu hao waliamua kuachana naye na kuendelea na mkakati wa kushusha majembe mengi  had hapo watakapojiridhisha kuwa  ndiye anayestahili  kwa mujibu wa vigezo anavyovitaka kocha Dylan Kerr.

No comments:

Post a Comment