Thursday, August 6, 2015

TANZANIA imeporomoka kwa nafasi 13 ndani ya miezi miwili hadi ya 140 katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Tanzania iliporomoja hadi nafasi ya 139 mwezi uliopita na mwezi huu imeporomoka kwa nafasi moja zaidi katika viwango vya FIFA, maana yake kidogo mambo yameanza kunyooka.
Juni mwaka huu baada ya matokeo mabaya mfululizo kuanzia kwenye Kombe la COSAFA ambako ilifungwa mechi zote tatu za Kundi B, mechi ya kwanza kufuzu AFCON ilipochapwa 3-0 na Misri kabla ya kutolewa kwa mabao 4-1 na Uganda kufuzu CHAN 2016, Tanzania iliporomoka kwa nafasi 12.
 

 Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa (kushoto) na Msaidizi wake, Hemed Morocco kulia
 
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likamfukuza kocha Mholanzi, Mart Nooij baada ya matokeo hayo na nafasi yake sasa anakaimu, Nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ambaye amepewa miezi mitatu ya majaribio.
Mkwasa alianza vizuri kwa sare ya ugenini ya 1-1 dhidi ya Uganda kufuzu CHAN na wakati wowote atataja kikosi cha kuingia kwenye kambi ya maandalizi ya mchezo wa pili kufuzu AFCON dhidi ya Nigeria mwezi ujao.
Kwa Afrika Mashariki na Kati, Uganda inaoongoza ikiwa nafasi ya 74 duniani, ikifuatiwa na Sudan 87, Rwanda 91, Ethiopia 99, Kenya 116, Burundi 132, Tanzania 140, Sudan Kusini 195, Eritrea 203, Somalia 204 na Djibouti 206.  
Kwa Afrika, Algeria bado inaongoza ikiwa nafasi ya 19 kwenye viwango vya dunia ikifuatiwa na Ivory Coast iliyo nafasi ya 20, Ghana 27, Tunisia 34 na Senegal 39.
Argentina inashika namba moja kwa ubora wa soka duniani ikifuatiwa na Ubelgiji, Ujerumani, Colombia na Brazil katika tano bora.

No comments:

Post a Comment