Beki katiri Simba aanika siri nzito
Na Majuto Mbiligenda
BEKI kisiki wa kikosi cha Wekundu wa Msimbazi Juuko Murshidi, maarufu kama ' Rio Ferdinand' ameweka hadharani kuwa uimara wake unatokana na kutumia akili nyingi na nguvu kidogo katika kuwakabili washambuliaji wa timu pinzani.
Kutokana na hilo ndiyo maana baadhi ya wachezaji wanadhani anacheza faulo, jambo ambalo anapingana nalo kwa kusema, hakuna beki yeyote duniani anayesifiwa kama walivyo wachezaji wa idara zingine uwanjani.
Kauli ya Juuko inakuja siku chache baada ya kuisaidia timu yake kushinda mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya SC Villa na URA zote zinatoka nchini Uganda ambako ndiko alikozaliwa beki huyo.
Katika mechi zote mbili, kikosi cha Simba kiliibuka na ushindi huku Juuko akionesha kiwango cha juu katika safu ya ulinzi akishirikiana vyema na Hassan Kessy ' Alves', Hassan Isihaka na Mohamed Hussein 'Tshabalala'.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Juuko alisema, kinachoonekana kama anacheza kibabe ni aina ya uchezaji wake wa kucheza kwa kutumia nguvu kidogo na kwamba hiyo ndiyo sifa ya mchezaji yeyote anayecheza kama beki wa kati.
Alisema, mchezaji wa safu ya ulinzi kamwe hawezi kusifiwa kwa kucheza kama mshambuliaji na ndiyo maana kuna msemo wa kwamba 'beki hasifiwi' bali hulaumiwa pindi anapopitwa na timu pinzani kushinda.
Aliongeza kuwa, aina ya uchezaji wake unawapa hofu washambuliaji wa timu pinzani kwasababu ya stamina aliyonayo, huku akimwaga sifa kemkem kwa kocha wa mazoezi ya viungo, Dusan Momcilovic na kusema amemuongezea nguvu na mbinu za kuhimili mikikimikiki ya washambuliaji wa timu pinzani.
"Ukiniangalia ninavyocheza utapata jibu kuwa huwa natumia akili nyingi na nguvu kidogo wakati ninapomkabili mchezaji wa timu pinzani, hapo ndipo utakaposikia ninacheza kibabe jambo ambalo siyo kweli".
"Hata hivyo lazima watu watambue kuwa mimi ni mchezaji wa idara ya ulinzi, lazima niwe na nguvu nyingi za kukabili mikikimikiki ya wachezaji wa safu ya ushambuliaji, nikicheza legelege sitakuwa na sifa za kuwa beki imara katika kikosi cha timu yangu".
"Lakini kubwa ambalo wengi hawajui ni kwamba mchezaji anayecheza nafasi ya ulinzi hayumo katika orodha ya wachezaji wanaoweza kusifiwa, kwani beki hawezi kusiwa hata siku moja" alisisitiza Juuko na kuongeza.
"Lingine ni kwamba, kocha wetu wa mazoezi,Dusan Momcilovic ametuongezea stamina za kutosha msimu huu ambapo kwasasa kila mchezaji ana uwezo wa kucheza hata dakika 120 bila ya kuchoka, tofauti hal ilivyokuwa msim uliopita ambao baadhi ya wachezaji walikuwa wanaonekana wanachoka mapema kipindi cha pili".
Juuko ndiye aliyeifungia timu ya Simba bao la pili katika mchezo wa Jumamosi iliyopita dhidi ya timu ya Watoza Ushuru wa Uganda, URA, ambapo Wekundu hao walitoka na ushindi wa mabao 2-1 huku bao la kwanza likipachikwa nyavuni na straika mpya Kelvin Ndayisenga, raia wa Burundi.
No comments:
Post a Comment