Thursday, September 10, 2015

Yanga yaweka kambi Kariakoo kujiandaa kuivaa Coastal Union Jumapili



MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga SC jana wameingia kambini katika hoteli ya Valley View, Mtaa wa Kongo, Kariakoo, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wao wa kwanza wa LIgi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union Jumapili.
Hoteli maridadi ya Valley View ipo jirani kabisa na makao makuu ya klabu ya Yanga SC, Jangwani na sababu kubwa za kambi kuwekwa hapo ni kuhakikisha wachezaji wanakuwa chini ya uangalizi mzuri.
Awali, Yanga SC ilipanga kuweka kambi katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani- lakini baada ya ushauri wa kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm imeamua kubaki Jijini.
Yanga SC wataanza na Coastal Union ya Tanga Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam- wakati mechi nyingine zote za ufunguzi zitachezwa Jumamosi.
Yanga SC iliuanza vizuri msimu baada ya kutwaa Ngao ya Jamii kwa ushindi wa penalti 8-7 dhidi ya Azam FC kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90- na sasa inaingia kwenye mbio za kutetea taji.
Kabla ya Yanga SC na Coastal Jumapili, mechi za ufunguzi za Ligi Kuu Jumapili zitakuwa kati ya 
Ndanda FC na Mgambo Shooting, African Sports na Simba SC, Majimaji FC na JKT Ruvu, Azam FC na Prisons, Stand United na Mtibwa Sugar, Toto Africans na Mwadui na Mbeya City na Kagera Sugar.

No comments:

Post a Comment