Saturday, September 19, 2015

Azam Tv yatoa ufafanuzi juu ya kuahirisha kuonesha mechi za Ligi Kuu

Mkurugenzi wa Masoko wa Azam TV, Mgope Kiwanga
 
KAMPUNI ya Azam TV inakanusha taarifa za kizushi zilizoenea kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kwamba kuna mpango wa kuahirisha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa ajili ya kuonyesha mechi za Ligi Kuu ya Hispania, La Liga.
Katika mkutano wetu na bodi ya Ligi kuu Tanzania (TPLB) tarehe 15 Septemba 2015, AzamTV iliiomba bodi kufikiria kubadili muda wa kuanza mechi za ligi katika siku za Jumamosi na Jumapili ili kuruhusu urushaji wa mechi nyingi zaidi za moja kwa moja (live). Hivi ndivyo jinsi ligi za nchi za barani Ulaya zinavyofanya ili kuhakikisha wapenzi wa soka wanashuhudia mechi kadhaa ndani ya siku moja. Kwa mfano, mechi tatu za EPL huruka muda tofauti katika siku moja.
Kama hapa nyumbani Tanzania, mechi za ligi nazo zingepangwa kuanza muda tofauti kama wanavyofanya wenzetu, kwa mfano mechi zingeanza saa 8:00 mchana, Saa 10:00 alasiri na saa 12:00 jioni, basi wapenzi wa soka wasingepata shida kuchagua mechi gani ya kuangalia na badala yake kuangalia mechi zote 3. Kuliko ambavyo watakapokuwa na wakati mgumu wikiendi hii ambapo mechi zote zitaanza saa 10:00 alasiri. 
Hii ina maanisha, si wapenzi wa soka tu watakaofaidika na mabadiliko haya, bali fursa hii ya kuonekana moja kwa moja (live) kwenye TV itaongezeka maradufu kwa wachezaji, klabu zao, pamoja na wadhamini wao. Vile vile hii inamaanisha kwamba sio timu kubwa tu zitakazofaidika, bali timu zote kwenye ligi ya VPL zitapata nafasi ya kuonyesha ujuzi wao mbele ya wadau na wapenzi wa soka.
Hizi mechi zitaonyeshwa kupitia chaneli ya Azam One na Azam Two ambazo mbali ya kupatikana ndani ya Tanzania, pia huonekana katika ukanda wote wa Kusini wa jangwa la Sahara katika nchi ambazo AzamTV inapatikana. Kwa hiyo kuongeza fursa ya kuonekana ndani na nje ya Tanzania. Tumefurahishwa na bodi ya Ligi kuu Tanzania kuonyesha ushirikiano katika kuunga mkono hoja hii na wataendelea kulifanyia kazi pamoja nasi ili kufanikisha ratiba ya aina hii.
Wateja wetu wa chaneli ya Azam Sports HD (ambayo inapatikana Tanzania tu) nao watapata fursa ya kuangalia baadhi ya mechi hizi katika ubora wa HD. Chaneli ya Azam Sports HD ni chaneli maalum inayoonyesha mechi za ligi ya Hispania (La Liga) ndani ya AzamTV. Hata hivyo taarifa za kizushi zilizoenezwa kwamba, tumependekeza ratiba hii ili kuitangaza zaidi La Liga kuliko VPL, hazina ukweli wowote. Mechi zote za Ligi kuu ya VPL zitarushwa kupitia chaneli zetu mbili za kimataifa – Azam One na Azam Two likiwemo pambano la watani jadi, Simba na Yanga Septemba 26, mwaka huu Saa 10:00 jioni kutoka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hii inamaanisha wateja wetu wote watapata nafasi ya muendelezo wa mechi kuanzia saa nane mchana mpaka saa sita za usiku kila mwisho wa wiki kwa kipindi chote cha msimu wa Tanzania, Afrika Mashariki na Hispania.

No comments:

Post a Comment