Klabu ya Simba imeeleza sababu za
kutomrejesha kundini mshambuliaji wake hatari Mkenya Paul Raphael
Kiongera ambaye mwishoni mwa mwaka jana alifanyiwa upasuaji wa goti
India.
Jumanne Agosti 12, 2014 Kiongera
(22) alisaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba kwa dau
lililoelezwa kuwa Dola za Marekani 20,000 (Sh. milioni 42), lakini
akaumia na kutonesha majeraha yake ya muda mrefu ya goti katika mechi
yao ya kwanza ya ligi ya Bara msimu uliopita waliyotoka sare ya 2-2
dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa.
Kaimu Katibu Mkuu wa Simba,
Collins Frisch, amesema jijini hapa kuwa hawana mpango wa kumrejesha
nchini mshambuliaji huyo kwa vile tayari ana mkataba wa miezi sita
kuitumikia kwa mkopo klabu ya KCB ya Ligi Kuu yta Kenya (KPL).
“Kuna mambo mengi yanazungumzwa
kuhusu Simba na Kiongera, lakini hayana ukweli. Watu wanasema Kiongera
ni mgonjwa akiwa Tanzania, lakini anatupia akiwa Kenya. Hatuwezi
kumrudisha kwenye kikosi chetu kwa sasa kwa sababu ana mkataba wa miezi
sita na KCB utakaomalizika Desemba,” amesema.
Mjumbe huyo wa Kamati ya Utendaji
ya Simba amesema Kiongera bado ni mali ya klabu hiyo ya Msimbazi kwa
muda mrefu kwani mkataba wake ulirefusha zaidi baada ya kuumia mwaka
jana.
Kabla ya kuumia, Kiongera
aliichezea Simba mechi tano tu na kufunga mabao mawili. Kwa sasa
anashika nafasi ya tano kwenye orodha ya wafumania nyavui hatari KPL
akiwa na mabao tisa, 10 nyuma ya kinara Jesse Were (Tusker FC)
anayefuatwa na mkali Micheal Olunga wa Gor Mahia mwenye mabao 15, Meddie
Kagere wa Gor Mahia pia (13) na John Makwata wa Ulinzi Stars (10).
No comments:
Post a Comment