Wednesday, September 2, 2015

Ngassa haelewe kinachoendelea Free State


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa amesema kwamba haelewei mustakabali wake sasa katika klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini baada ya ujio wa kocha mpya, Mjerumani Ernst Middendorp.
Akizungumza baada ya kuwasili Dar es Salaam kujiunga na timu ya taifa, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya Nigeria mwishoni, Ngassa amesema yuko njia panda.
“Haimaanishi kwamba mambo magumu au nimekata tamaa, hapana bali naihisi changamoto mpya iliyopo mbele yangu kutokana na desturi za makocha wengi duniani,”amesema.
“Unajua kila kocha anapoingia katika timu anaingia na falsafa zake na anakuwa na aina ya wachezaji ambao anaona watamfaa. Sasa sijui kama mimi nitakuwa miongoni mwa atakaoona wanamfaa,”ameongeza Ngassa.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga SC amesema alisajiliwa Free State na kocha Mmalawi, Kinnah Phiri ambaye amejiuzulu wiki iliyopita na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani huyo.
“Kinnah alikuwa ananikubali na wakati wote ndani na nje ya Uwanja alikuwa ananipa moyo nijitahidi nitaiweza soka ya Afrika na nitakuwa nyota. Nilikuwa nasikia raha sana kuwa katika ile timu na yeye akiwa kama baba yangu pale. Sasa ameondoka, sijui itakuwaje,”amesema.
Baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo za mwanzo za Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini, 1-0 kutoka kwa Mpumalanga Blac Aces, 4-0 kutoka kwa Kazier Chiefs na 2-1 mbele ya Ajax Cape Town, Phiri ameondoka na nafasi yake anachukua Middendorp.
Middendorp ni kocha wa zamani wa Kaizer Chiefs na Bloemfontein Celtic, ambaye alikuwa anafundisha Chippa United msimu uliopita.
Mjerumani huyo aliwaacha katika mazingira mabaya Chilli Boys baada ya kusimamishwa Machi kufuatia matokeo mabaya kwa timu hiyo ya Port Elizabeth.
Ngassa alisajiliwa Mei mwaka huu na Free State ya Bethelehem baada ya kocha Phiri kuvutiwa na soka yake akiwa anacheza Yanga SC ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment