Wednesday, September 23, 2015

Lewandoski apiga bao 5 akitokea benchi na kuweka rekodi

Robert 
Wakati Bayern Munich ikiwa nyuma kwa goli 1-0 hadi mapumziko kwenye uwanja wake wa nyumbani, Robert Lewandowski aliingia akitokea benchi na kubadilisha matokeo ya mchezo huo kwa kufunga magoli matano ndani ya dakika tisa kwenye mchezo dhidi ya Wolfsburg uliomalizika kwa Bayern kuibuka na ushindi wa goli 5-1.
Mabingwa hao wa Bundesliga waliingia kwenye mechi hiyo dhidi ya Wolfsburg ambayo ilimaliza ikiwa nafasi ya pili msimu uliopita walianza kuduwazwa kwa goli la Daniel Caligiuri la kipindi cha kwanza na kumfanya Pep Guardiola kufanya mabadiliko mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Kocha huyo wa Bayern alimpumzisha kiungo Thiago Alcántara na kumuingiza Lewandowski.
Mkali huyo mwenye miaka 27 ilimchukua dakika sita pekee kuisawazishia Bayern baada ya kuunasa mpira kutoka kwa mchezaji mwenzake wa zamani Dante na kuiandikia Bayern bao la kusawazisha kabla ya kuiweka timu yake mbele dakika moja baadae kwa shuti kali la nje ya boksi.
Lewandowski alikamilisha hat-trick yake dakika nne baadae na kuweka rekodi ya kuwa hat-trick ya haraka zaidi kufungwa kwenye historia ya Bundesliga. Rekodi ya hat-trick ya mapema ilikuwa ikishikiliwa na Michael Toennies iliyowekwa mwaka 1991 ndani ya dakika sita. 
Rekodi yake ya mabao matano kwenye mechi moja ni ya haraka zaidi mara nne ya ile iliyowekwa na Jermain Defoe mwaka 2009 Tottenham iliposhinda kwa goli 9-1 dhidi ya Wigan.
Dakika mbili baadae baada ya kufunga hat-trick, Lewandowski alifunga goli la nne akiunganisha krosi ya mchezaji mpya aliyesajiliwa kwenye klabu hiyo Douglas Costa kabla hajapiga goli la tano kwa staili ya ‘bicycle kick’ akiwa nje kidogo ya boksi na kumwacha Guardiola akitabasamu.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund anakuwa mchezaji wa kwanza wa Bayern kufunga magoli matano ndani ya Bundesliga tangu alipofanya hivyo Dieter Hoeness mwaka 1984.
Lewandowski pia amekuwa mchezaji wa kwanza aliyetokea benchi na kufunga magoli matano.

No comments:

Post a Comment