Taasisi ya GSM Foundation ya Dar
es Salaam imetoa Sh milioni 50 kwa ajili ya kudhamini tuzo za
wanamichezo waliofanya vizuri zaidi katika miaka 10 ya uongozi wa Rais
Jakaya Kikwete.
Utoaji wa tuzo hizo utafanyika
Oktoba 8, mwaka huu ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ambapo
wanamichezo pia watatumia tuzo hizo zilizoandaliwa na Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kumuaga Rais Kikwete
anayemaliza muda wake kikatiba.
Kwa mujibu wa TASWA licha ya
kumuaga Rais Kikwete na kutoa tuzo kwa wanamichezo 10 waliofanya vizuri
zaidi, pia chama hicho kitatoa Tuzo ya Heshima Rais Kikwete ikiwa ni
kuthamini mchango wake kwa michezo katika utawala wake.
Akizungumza katika mkutano na
waandishi wa habari kutambulisha udhamini huo Dar es Salaam jana,
mwakilishi wa GSM Foundation, Elibariki Lukumay, alisema wameguswa na
tukio hilo na kuona kuna umuhimu wa kuiunga mkono TASWA.
“Taasisi yetu ambayo ina kampuni
mbalimbali imeguswa na kitendo ambacho TASWA inakiandaa na kwa kuanzia
tunatoa kiasi hicho cha fedha kufanikisha jambo hilo na tunawaomba
wengine pia waunge mkono.
“Rais Kikwete amefanya mambo
makubwa katika michezo nchi hii, hivyo tukiwa pia wadau wakubwa wa
michezo tumeona ni vyema tuungane na wenzetu wa TASWA katika kumuaga na
kumshukuru kwa mchango mkubwa alioufanya kwa michezo,” alisema Lukumay.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
TASWA, Juma Pinto aliishukuru taasisi hiyo na kusema kuwa bajeti ya
tukio hilo ni Sh milioni 130 na kwamba wadhamini hao wamefungua milango
kwa wengine ili kulifanikisha jambo hilo.
“Tunaamini mchango wa Rais
Kikwete katika medani ya michezo hauna mfano na kila mdau wa michezo
atakubali amefanya mambo makubwa kwa michezo.
“Tunafahamu Rais alivyosimamia
serikali yake kulipia makocha wa michezo ya soka, netiboli na ngumi. Pia
chini ya utawala wake serikali ilipeleka wanariadha wetu China,
Ethiopia na New Zealand kwa maandalizi ya mashindano ya kimataifa,”
alisema.
Alifafanua kuwa karibu vyama
vyote vya michezo nchini vitashikirikishwa katika tukio hilo ikiwa ni
pamoja kuwa karibu kwa kila hatua na Wizara Ya Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
No comments:
Post a Comment