Saturday, September 19, 2015

Amokachi aacha kazi baada ya wiki tano




NAHODHA wa zamani wa Nigeria, Daniel Amokachi amejiuzulu wadhifa wake kama meneja wa klabu ya ligi kuu ya Nigeria, FC IfeanyiUbah baada ya kuiongoza kwa wiki tano pekee.
Amokachi mwenye umri wa miaka 42 alikuwa awali ameeleza hamu yake ya kutaka kushinda mataji na kuhakikisha klabu hiyo.
Lakini ameamua kuondoka baada ya msururu wa matokeo mabaya na kutoelewana kati yake na mmiliki wa klabu hiyo.
“Nasikitika kuondoka baada ya kipindi kifupi hivi, lakini kandanda inaendelea,” alisema Amokachi akiiambia BBC Sport.
“Nilikuwa shabiki wa Klabu hii kabla ya kuteuliwa kwangu kama meneja kwa sababu ya msingi uliopelekea kuundwa kwake.
"Lakini sasa naitakia kila la heri na nitafuatilia hatua wanazopiga kwa fahari kuu.”
Ripoti zimedokeza kuwa Amokachi hakufurahishwa na sera ya klabu hiyo ya kutumia barabara hatari usiku kurejea nyumbani baada ya kucheza mechi za ugenini.
Msimamo wake ulimfanya kukosana na milionea anayemiliki klabu hiyo, Ifeanyi Ubah.
Mfanyabiashara huyo anaaminika kuchukulia hatua ya kocha huyo kuwa kukaidi mamlaka yake.
Amokachi alikataa kusema lolote alipoulizwa kuhusu suala hilo.
“Soka haitabiriki na hakuna wakati wa kwenda mbele na nyuma,” alisema.
"Imekuwa heshima kubwa kuhusika katika kilabu hii lakini kwa sasa safari yangu imefikia kikomo FC IfeanyiUbah."

No comments:

Post a Comment