Saturday, September 5, 2015

Wachezaji waliofanyiwa figisufigisu dakika za mwisho za usajili

de Gea asalia 
Mambo vipi ndugu zangu popote mnaposoma habari hizi bila shaka mmeanza kuwa wastaarabu baada ya ile sheria kuanza kutumika japokuwa sina uhakika sana kama tukiwazungumzia akina Bafetimbi Gomiz bila kuwataja majina sheria hii itatuhusu. Anyway ‘Itafahamika’ ila kwa leo naomba tuangalie sajili ambazo  zilikwama dakika za mwisho na kuhusishwa na figisufigisu kibao kutoka pande fulani fulani, karibu kutazama hapa chini…
FABIO COENTRAO
Mwaka 2013 beki huyu wa kushoto alihusishwa kuhamia Old Trafford. Timu za Real Madrid na Man U zilishakamilisha kila kitu ila kosa walilolifanya ni kuchelewa kukusanya nyaraka za usajili kwa wakati. Kipindi hiki Man U walikuwa na mabeki wa kushoto, Patrice Evra na Alexander Buttner, kitu hiki ndicho kilikuwa kinawapa kiburi kuchelewesha nyaraka hizi hadi dirisha kufungwa. Pia United walipewa kiburi na beki Leighton Baines wa Everton kwani kipindi hiki walikuwa wanaamini watanasa saini yake.
JOAO MOUTINHO
Kiungo wa kimataifa kutoka Ureno alitarajiwa kusaini Tottenham mwaka 2012 wakati timu hii ipo chini ya Meneja Andre Villas Boas. Wakati Spurs ikidhani imempata mrithi wa Luca Modric, madudu ya dakika za mwisho yalikwamisha uhamisho huu na kupelekea Moutinho kwenda Monaco. Inasemekana Spurs walikamilisha taarifa saa 3 usiku ila majadiliano yalikwenda hadi saa 7 usiku na hatimaye tarehe 1 September kufika bila maafikiano kufika baina ya timu zote. Kulikuwa na majadiliano ya pande 3, vilabu viwili na ule upande wa mmiliki wa mchezaji. Mwisho wa siku usajili huu ulikwama dakika za mwisho.
ANDER HERRERA
Japokuwa kwa sasa ni mchezaji wa Manchester United, ila alipaswa kuhamia kwenye timu hii mapema sana mwaka 2013 lakini Atletco Club Bilbao ilipishana na Man U dakika za mwisho na hatimaye uhamisho huu kukwama mwaka 2013. Inaelezwa timu hizi zilishindwana kwenye maafikiano ya bei licha ya wanasheria wa vilabu hivi kukutana mara kwa mara. Baada ya dili hili kukwama kipindi cha kiangazi hatimaye mwaka 2014 Man U ilimnasa mchezaji huyu na kwa sasa ameingia kwenye vitabu vya wachezaji waliosajiliwa na Man U.
YEVHEN KONOPLYANKA
Winga huyu kutoka Ukraine alihusishwa na kuhamia Anfield mwaka 2014 na tayari baadhi ya makaratasi yalisha sainiwa na vilabu hivi viwili vya Liverpool na Dnipro. Mmiliki wa Dnipro tayari alishatangaza muda wowote winga huyu atakwenda Liverpool. CEO wa Liverpool Ian Ayre tayari alitarajiwa kwenda Ukraine kukamilisha kila kitu kabla dirisha halijafungwa ila cha kushangaza uhamisho huu ulikwama dakika za mwisho hadi dirisha linafungwa. Liverpool walikwama kumpeleka mchezaji huyu Merseyside kutokana na uzembe mwishoni kabisa.
DAVID DE GEA
Huu ni mfano mzuri kwa kipindi hiki kwani ilifikia hatua ya mlinda mlango huyu kutaka kuuza kila kitu pale Uingereza kwa kuamini kuwa anakwenda kwao Hispania ila dakika ya mwisho kabisa mambo yalikwenda kombo. Kuna mambo mengi yalitokea juu ya uhamisho huu ila suala la ada ya uhamisho lilichelewesha usajili huu na makubaliano ya dakika za mwisho yalifanya muda kutokuwa rafiki na hatimaye usajili huu kuwa ndoto. Kila timu imeonekana kutoa lawama kwa mwenzake na ukweli unabaki kuwa dakika za mwisho mambo ndio yaliharibika kabisa.

No comments:

Post a Comment