Wednesday, September 2, 2015

Nigeria kutua Dar kesho tayari kuivaa Stars

Kikosi cha timu ya Taifa ya Nigeria 'The Eagles'
Kama ulikuwa hujui, wanakuja Alhamisi!  Wapinzani wa Taifa Stars katika kuwania tiketi ya kufuzu kushiriki fainali zijazo za Mataifa ya Afrika (Afcon), Nigeria watatua jijini Dar es Salaam Alhamisi. Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) limetangaza rasmi kuwa kikosi cha Super Eagles kwa ajili ya mechi ya Jumamosi dhidi ya Taifa Stars kitaondoka Abuja kesho saa 9 jioni kwa saa za Nigeria (saa 7 mchana kwa saa za Tanzania). 
Kwa mujibu wa taarifa ya NFF iliyowekwa kwenye mtandao rasmi wa shirikisho hilo leo alasiri, mabingwa hao mara tatu wa Afrika watatua kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini hapa saa 4 usiku kwa saa za Tanzania (saa 2 usiku kwa saa za Nigeria). 
Msafara wa Supper Eagles utakuwa na wachezaji 23, maofisa wa benchi la ufundi, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya NFF na maofisa wa serikali ya Nigeria, maofisa wa NFF, waandishi wa habari,wadau wa soka wa Nigeria na wajumbe wa klabu ya mashabiki wa soka wa Nigeria. 
Nchi hizo mbili hazijawahi kukutana katika michuano hiyo mikubwa barani tangu Desemba 1980, lakini zimekuwa zikichuana katika michuano ya vijana na soka la wanawake katika miaka ya karibuni. 
Desemba hiyo ya miaka 35 iliyoipita Taifa Stars ina matumaini ya kufanya kweli kutokana na kuwashika Green Eagles (kipindi hicho) kwa sare ya 1-1 jijini Lagos katika mechi yao ya kwanza ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 1982, lakini magoli mawili ya kipindi cha kwanza yaliyofungwa na John Chidozie na Christian Nwokocha jijini Dar es Salaam wiki mbili baadaye yaliisukuma Tanzania nje ya michano. 
2011 timu ya taifa ya Nigeria U-23 ilipoteza 0-1 dhidi ya Tanzania katika hatua ya mchujo ya michuano ya 2012 ya Olympics, lakini ikashinda 3-0 jijini Benin.
Mwaka uliofuata Flying Eagles ikaing’oa timu ya taifa ya Tanzania ya U-20 ‘Ngorongoro Heroes’ kwenye mbio za kuwania kushiriki michuano ya vijana ya Afrika 2013. 
Mwaka jana Super Falcons ilizima ndoto za Twiga Stars kushiriki michuano ya tisa ya Afrika kwa Wanawake iliyofanyika Namibia. 
Mechi ya kukumbukwa zaidi kati ya Taifa Stars na Supper Egles ni ile ya kirafiki ya Julai 6, 1972 zilipotoka suluhu jijini Dar es Salaam. Miezi minne baadaye Eagles walicheza mechi mbili za kirafiki na kushinda 2-1 na 3-2 jijini Benin na Lagos, kisha kushinda tena 2-1 dhidi ya Taifa Stars wakati wa raundi ya pili ya mashindano ya All-Africa Games ambayo Nigeria ilikuwa mwenyeji Januari 1973. 
Februari 1976, timu hizo zilitoka suluhu katika mechi ya kirafiki jijini Dar es Salaam wakati Green Eagles ilipopita kuelekea Ethiopia kwenye michuano ya Afcon. 
Taifa Stars inatarajiwa kutua nchini usiku wa kuamkia kesho ikitokea kambini nchini Uturuki.

No comments:

Post a Comment