Nikiwa naamini hali yako ni njema, mimi pia ni mzima kiasi ila nasikitika yanayotokea pale Saudia huku nikiwaombea Marehemu wote wawe salama huko waliko. Tukirejea katika soka, naamini habari ya mujini ni Lewandowski hasa baada ya kufunga magoli 5 pale timu yake ya Bayern Munich ilipo toa kisago cha 5-1 dhidi ya timu ngumu ya Wolfsburg. Kutokana na hili leo nimekuwekea listi ya Wachezaji wengine ambao wamewahi kufunga magoli 5 katika mechi 1, karibu sana kuungana na mimi hapa chini…
ROBERT LEWANDOWSK
Huyu jamaa ni mchezaji hatari
sana ambaye kufunga goli inawezekana ndiyo kazi rahisi kuliko hata
kuvuta pumzi. Aliwahi kuwafunga Real Madrid magoli 4 kwenye UEFA na hapo
dunia ya soka ikaamini kuwa huyu jamaa anaweza kutoa dozi kubwa zaidi
endapo atapewa upenyo wa kufanya hivvo. Baada ya Wolfsburg kujichanganya
kwenye mechi ya Bundesliga siku kadhaa zilizopita, Lewandowski alitupia
magoli 5 peke yake tena ndani ya dakika 9 huku akikamilisha ‘hat trick’
yake ndani ya dakika 3 na sekunde 22. Kumbuka aliyafanya haya baada ya
kutokea benchi huku Bayern ikiwa nyuma kwa goli moja.
LUIZ ADRIANO
Ni
kijana mdogo ambaye hivi karibuni aliandika rekodi ya kufunga magoli 5
katika mechi 1 ya UEFA. FC BATE Borisov ilimruhusu Adriano kufunga
magoli 5 mwaka 2014 wakati Shakhtar Donetsk ilipocheza na timu hii na
kushinda magoli 7 huku Mbarizil huyu akitupia magoli 5 kwenye usiku wa
UEFA na kuandikwa kwenye vitabu vya historia sambamba na mchezaji bora
wa Ulaya Lionel Messi ambaye tayari alishawahi kufanya hivi kipindi cha
nyuma. Luiz Adriano licha ya kufunga magoli haya, hakufanikiwa kuwa
mfungaji bora wa Ulaya kwa kipindi cha 2014.
MIROSLAV KLOSE
Ni
Mchezaji mwenye busara sana ila Bologna hawatamsahau mwaka 2013 pale
ambapo Klose alifunga magoli 5 katika ushindi wa 6-0 walioupata Lazio
kwenye mechi ya ligi kuu ya Italia. Klose ni mmaliziaji mzuri sana
japokuwa hakujaaliwa chenga wala mbio ila amepewa macho ya ziada ya
kutambua nyavu zilipo. Hadi sasa Klose anashikilia rekodi ya kuwa
mfungaji bora wa muda wote kwenye michuano ya kombe la dunia baada ya
kumpiku nguli wa soka Ronaldo de Lima.
FERNANDO MORIENTES
Naamini
Liverpool wanamfahamu vyema kwani ameshacheza Anflied na kushindwa
kuwika kama alivyokuwa Hispania. Las Palmas walifungwa 7-0 na Real
Madrid mwaka 2002 huku Morientes akitia kambani magoli 5 na kuwa
miongoni mwa Wanasoka waliocheza Madrid na kutupia magoli 5 katika mechi
1. Katika mechi hii nakumbuka Morientes alikosa nafasi ya kutupia
magoli 6 baada ya kukosa mkwaju wa penati.
ALAN SHEARER
Hakuna asiyefahamu makubwa
aliyofanya huyu jamaa katika ligi kuu ya Uingereza. Mwaka 1999,
Newcastle iliinyuka Sheffield Wednesday 8-0 huku Shearer akiingia
nyavuni mara 5. Japokuwa alifunga penati 2 katika magoli yake ila hadi
sasa Shearer anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote
katika ligi kuu ya Uingereza na timu yake ya Newcastle.
OLEG SALENKO
Japokuwa wengine tulikuwa kwenye
‘Mabeseni’ ila Ulimwengu wa digitali unatuwezesha kumfahamu huyu jamaa
zaidi. Salenko aliwafunga Waafrika magoli 5 baada ya Urusi kuibamiza
Cameroon magoli 6-1 kwenye michuano ya kombe la dunia pale Marekani.
Hadi sasa rekodi hii haijavunjwa katika michuano hii licha ya miaka 20
kupita tangu Mshambuliaji huyu kufanya unyama huu kwa Waafrika na
kuidhihirishia Dunia kuwa Afrika kisoka bado sana. Kutokana na magoli
yake, Salenko alifanikiwa kuwa mfungaji bora wa michuano hii ambayo
Brazil ilifanya makubwa.
JERMAIN DEFOE
Akiwa
katika ubora wake mwaka 2009, Defoe alitupia magoli 5 pale timu yake ya
Spurs iliposhinda 9-1 dhidi ya Dearby Country. Defoe alicheza kwa
mafanikio ya wastani katika timu ya Spurs kitu ambacho kilimsaidia
kuweka rekodi hii ya kiume ambayo kila mchezaji anatamani kuitekeleza
kabla hajastaafu.
LIONEL MESSI
Alifanya
makubwa kwenye usiku wa Uefa mwaka 2012 pale ambapo wachezaji wa Bayer
Leverkusen walipompa uhuru na kusahau makali ya mchezaji huyu ambaye
inasadikika ndiye bora kuwahi kutokea hapa Duniani. Barcelona iliiadhibu
Leverkusen magoli 7-1 kwenye mzunguko wa pili wa hatua ya 16 bora huku
Mchawi Messi akimpa kazi mlinda mlango wa Leverkusen kuokota mipira mara
5. Kutokana na magoli haya, Messi alikuwa Mchezaji wa kwanza kufunga
magoli 5 katika mechi moja ya UEFA.
RADAMEL FALCAO
Anabezwa
sana kwa sasa ila ni Mchezaji aliyeweka rekodi nyingi wakati akiwa
katika ubora wake. Ikumbukwe Mwaka 2012 akiwa Atletco de Madrid, Falcao
aliwafunga Deportivo la Coruna magoli 5 pale ambapo ‘Superdepo’ walilala
6-1 kwenye La liga. Falcao alikuwa mchezaji hatari ambaye anawaumiza
akili mabeki wa timu pinzani kutokana na utaalamu wake wa kufumania
nyavu. Kwa sasa yupo Chelsea na bado anadharaulika kutokana na kushuka
kiwango.
DIMITAR BERBATOV
Baada
ya kuondoka Spurs na kwenda United, hatimaye Mchezaji huyu akiwa Old
Trafford alitupia magoli 5 pale ambapo United iliinyuka Blackburn Rovers
magoli 7-1. Mbulgaria huyu hakupata mafanikio sana akiwa na uzi
mwekundu wa United licha ya kufahamika kama miongoni mwa wamaliziaji
wazuri hadi sasa licha ya umri wake kusogea.
CRISTIANO RONALDO
Huyu
jamaa mimi namuheshimu na kumuogopa sana kwani anaamua afunge magoli
mangapi katika mechi gani. Cr7 ana uwezo wa kufunga idadi yoyote ya
magoli atakayo. Miezi michache iliyopita Madrid ilishinda 9-1 dhidi ya
Granada huku Cr7 akiingia nyavuni mara 5 na kuendelea kuandika rekodi
mbalimbali ikiwemo ile ya kufunga ‘hat-trick’ ndani ya dakika 18.
Ronaldo ni mchezaji hatari ambaye kwa sasa anainyemelea rekodi ya kuwa
mfungaji bora wa muda wote pale Real
Madrid.
Madrid.
No comments:
Post a Comment