Wednesday, September 9, 2015

Kocha Simba apanga kuifanyia kweli African Sports


KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Muingereza, Dylan Kerr, amesema kwamba kikosi chake kimepanga kufanya vizuri katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ambayo inatarajiwa kuanza Jumamosi kwa kupata ushindi wa 'kihistoria' ugenini itakapokabiliana na wenyeji African Sports kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini, Tanga.
Kerr alisema kwamba amekuwa anataka kuona Simba inashinda Jumamosi na kuendeleza rekodi yake ya kushinda mechi ya kwanza 'muhimu' kwa kuijenga timu kama ilivyokuwa katika Tamasha la Simba Day ilipofanikiwa kuwafunga URA wa Uganda.
Muingereza huyo alisema kwamba amewapa wachezaji wake mbinu mbalimbali za kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ya kwanza ili wapate nguvu ya kupambana mechi inayofuata.
"Mechi mbili ugenini ni ngumu, ila ukishinda ya kwanza, inayofuata pia unakuwa umejipanga zaidi, na unawapa hofu wapinzani, tunaendelea na mazoezi kwa sababu lengo letu ni kusaka ushindi", alisema Kocha huyo.
Kocha Kerr akiwa na Wasaidizi wake, amepania kuanza ligi kwa kishindo
 
Katika kuhakikisha kwamba wamedhamiria kushinda, uongozi wa Simba ulimsafirisha Kerr na Msaidizi wake, Selemani Matola, Jumapili kwenda Tanga kwa lengo la kuipelekeza African Sports ambayo ilikuwa inacheza mechi ya kirafiki na Coastal Union.
Simba imeweka kambi Visiwani Zanzibar na inatarajia kuondoka Visiwani humo keshokutwa Alhamisi asubuhi kuelekea Tanga tayari kwa mchezo huo utakaofanyika Jumamosi na kubaki jijini humo kuwasubiri Mgambo Shooting hapo Septemba 16 mwaka huu.
Kerr alipewa jukumu la kuiongoza Wekundu wa Msimbazi baada ya kuamua kuachana na Mserbia, Kopunovic, ambaye alimaliza msimu uliopita akiwa nafasi ya tatu.

No comments:

Post a Comment