Saturday, October 17, 2015

Ukiacha Uholanzi, hizi ni timu nyingine ambazo hazijafuzu

FBL-EURO-2016-NED-CZE 
Usiku Oktoba 13, 2015 ni wa kukumbukwa sana na wapenzi wa soka duniani hasa kwa wale mashabiki wa timu ya taifa ya Uholanzi maarufu kama ‘Orange’.
Timu ya taifa ya Uholanzi imeshindwa kufuzu michuano ya Ulaya baada ya kufungwa na timu ya taifa ya Jamhuri ya watu wa Czech kwa bao 3-2 katika uwanja wa Amsterdam Arena, Uholanzi.
Ilikuwa ni simanzi kubwa sana nchini Uholanzi, kichapo chao kimeifanya timu hiyo ishike nafasi ya nne katika kundi A lililokuwa na timu kama Jamhuri ya watu wa Czech, Island, Uturuki, Kazakhstan, Latvia na Uholanzi yenyewe.
Timu ambazo zimefuzu katika kundi hilo ni Island, Jamhuri ya watu wa Czech na Uturuki. Ni miaka 31 tangu kwa mara ya mwisho Uholanzi kushindwa kufuzu kwenye michuano ya Ulaya ya mwaka 1984 iliyofanyika nchini Ufaransa. Na mwaka huu 2015, Uholanzi imeshindwa kufuzu michuano ya Ulaya itakayofanyika Ufaransa mwaka 2016.
Uholanzi si nchi ya kwanza kushindwa kufuzu michuano mikubwa ya soka duniani, zipo pia nchi nyingine ambazo zimewahi kushindwa kufuzu michuano mbalimbali ya soka angali nchi hizo zikiwa na majina makubwa sana katika mchezo huo.
  ENGLAND
Baada ya kutwaa ubingwa wa dunia mwaka 1966 bado walishindwa kufuzu kucheza michuano ya kombe la dunia ya mwaka 1974 iliyofanyika nchini Ujerumani Magharibi baada ya kushindwa kuifunga timu ya taifa ya Poland katika uwanja wa Wembley.
England walishindwa pia kufuzu michuano ya kombo la dunia mwaka 1978 iliyofanyika nchini Argentina kabla ya kushindwa kufuzu fainali za kombe la dunia fainali za mwaka 1994.
Chini ya kocha Stive McLaren England ilishindwa kufuzu michuano ya Ulaya mwaka 2008 iliyofanyika katiika nchi za Austria na Uswis baada ya kufungwa na Croatia kwa goli 3-2 mwaka 2007.
SCOTLAND
Ikiwa na nyota wengi wa Celtic waliotwaa kombe la washindi barani Ulaya mwaka 1967 ilishindwa kufuzu michuano ya kombe la dunia mwaka 1970 iliyofanyika nchini Mexico. Scoland ilikubali kichapo cha goli 2-0 kutoka kwa Austria uliofanyika mjini Viena na kufuta ndoto za timu hiyo kushiriki michuano ya kombe la dunia.
UHOLANZI
Dunia ilipata mshtuko katika michezo ya kufuzu kucheza michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2002 baada ya timu ya taifa ya Uholanzi kushindwa kufuzu kwenye michuano hiyo iliyoandaliwa kwa pamoja na nchi za Japan na Korea Kusini.
Uholanzi ya wakati huo iliyokuwa na nyota wengi kama Ruud van Nistelrooy, Patrick Kluivert, Edger Davis na wengine chini ya kocha Louis van Gaal. Uholanzi ilishika nafasi ya tatu katika kundi lake nyuma ya Jamhuri ya watu wa Ireland ambao waliongoza kundi.
URENO
Mkasa wa kushindwa kufuzu kwenye michuano mikubwa pia umeikumba timu ya Ureno, timu hiyo iliyokuwa na kikosi cha dhahabu wakati huo miaka ya 1990 mpaka 2000 ilishindwa kufuzu michuano ya kombe la dunia iliyofanyika nchini Ufaransa mwaka 1998.
Nyota wa Ureno wa wakati huo alikuwa ni Louis Figo na wengineo walishindwa kuipeleka nchi yao katika fainali za kombe la dunia nchini Ufaransa.
UFARANSA
Ufaransa nao wapo katika kundi hilo kwa kukosa michuano ya kombe la dunia baada ya kukosa kushiriki fainali za mwaka 1994 zilizofanyika Marekani. Ikiwa na nyota kama Didier Deschamps (kocha wa sasa wa timu ya taifa ya Ufaransa), na Eric Cantona ilihitaji pointi moja tu katika michezo miwili dhidi ya Bulgaria na Israel.
Chakushangaza ni kwamba, Ufaransa ilipoteza michezo yake yote na kushindwa kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 1994.

No comments:

Post a Comment