Saturday, October 3, 2015

Taarifa ya Mbeya City FC kwa vyombo vya habari

"Bodi ya klabu ya Mbeya City ilikutana tarehe 29.09.2015 kwa dharula kulijadili suala ambalo hivi sasa linaendelea kujadiliwa katika Umma wa wanamichezo nchini likimuhusisha mchezaji wa timu yetu Juma Said maarufu kama “Nyoso” baada ya mchezo kati ya timu yetu na Azam Fc uliochezwa tarehe 27.9.2015 katika uwanja wa chamazi. 
 
Katika kikao hicho yafuatayo yaliamuliwa:
1. Klabu iliunda kikosi kazi kuliangalia suala zima na kikosi kazi hicho kilipewa masaa 86 na kilifanya kazi kwa adidu za rejea zifuatazo:
(a) Kupitia rejea za mchezo husika na kuangalia Mazingira na Asili ya suala zima lililojitokeza.
(b) Kupata Maelezo ya awali ya mchezaji wetu juu ya suala lenyewe.
(c) Kufanya uchambuzi wa kisayansi wa mzizi wa suala analohusishwa mchezaji kwa kushirikisha watalaam wa Ushauri Nasihi na Saikolojia kisha kuishauri Bodi.
Wakati kazi hiyo ikiendelea, Klabu ilipokea nakala ya barua ya adhabu ya mchezaji wetu Juma Said maarufu kama “Nyoso” yenye Kumb:TPLB/VPL/766/15 ya tarehe 30.09.2015.
Kwa Mukhtasari ifuatayo ni taarifa ya klabu baada ya kikosi kazi hicho kuwasilisha taarifa yake.
Klabu inapenda umma wa wanamichezo nchini ukajua kuwa inasononeka sana na matukio yoyote yenye kuupunguzia ladha mchezo wa mpira wa miguu kunakofanywa na mdau yoyote wa mchezo huo.
Mara zote klabu imekuwa ikisisitiza na kusimamia nidhamu ya wachezaji na viongozi muda wote wanapotekeleza majukumu yao.
Katika mchezo wetu wa ligi kuu namba 32 uliochezwa katika uwanja wa Chamazi tarehe 27.09.2015 inadaiwa mchezaji wetu tajwa hapo juu alifanya kitendo cha udhalilishaji dhidi ya mchezaji wa Azam Fc John Bocco.
Tarehe 29.09.2015 kamati ya masaa 72 inayoisimamia shughuli za bodi ya ligi ilikutana na kutoa uamuzi wa kumfungia mchezaji Juma Saidi Nyoso kutocheza mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka miwili na faini ya shilingi milioni mbili kwa kufuata kanuni namba 37(24) za ligi kuu toleo la 2015(Kwa mujibu wa barua TPLB/VPL/766/15 ya tarehe 30.09.2015).

Ufuatao ni uchambuzi wa adhabu iliyotolewa
1. (a) Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa bodi ya ligi ( Masaa sabini mbili) pamoja na mambo mengine inashughulikia kufanya maamuzi kwa masuala yote ambayo maamuzi yake hayakatiwi rufaa kama yalivyoainishwa katika kanuni namba 74 ya ligi kuu. Kanuni iliyotumika kutoa adhabu 37(24) si miongoni mwa kanuni ambazo hazikatiwi rufaa ni kanuni inayopaswa kutumika na kamati ya Maadili au Nidhamu ambayo kulingana na aina ya kosa linahitaji kuthibitishwa pasipo shaka na pande zote zinazohusika.
(b) Hata kama kanuni waliyoitumia ingekuwa ni sahihi lakini tafsiri ya kanuni hasa maneno AU, NA hayakutumika ipasavyo kwa kuwa walikuwa na uchaguzi wa adhabu lakini adhabu hizo haziendi pamoja kama kamati ilivyo tafsiri. Adhabu imeangalia upande mmoja wa hisia , hivyo kutoa adhabu kubwa bila kuangalia upande wa mchezaji husika. Pia Kamati imeunganisha adhabu zote kwa pamoja wakati kanuni inatoa nafasi ya adhabu moja kwa wakati mmoja.
“37(24) Mchezaji yeyote atakayepatikana na hatia ya kufanya makosa makubwa ya kimaadili au kinidhamu, au ya kibaguzi au yakidhalilishaji au yatakayotafsiriwa kuwa ni ukiukaji mkubwa wa taratibu za mchezo na ubinaadamu atatozwa faini kati ya shilingi milioni moja mpaka milioni tatu au/na kusimamishwa kushiriki michezo mitatu mpaka kumi ya klabu yake yoyote atakayoitumikia katika Ligi Kuu na mashindano mengine rasmi ya TFF  au kufungiwa kipindi cha kati ya mwaka mmoja na miwili.”
2. (a) Klabu inapata shaka juu ya maamuzi ya kamati husika kutokana na kikao kilichotoa maamuzi kiliongozwa na Mwenyekiti wa kamati hii ni Ndugu Said Mohamed ambaye pia ni Mwenyekiti wa Azam Fc. Sisi tuna amini kwamba kwa kuwa yeye ni kiongozi wa Timu ya Azam aliwajibika kujitoa kusikiliza shauri.Lakini hakujitoa na aliendelea kuongoza kikao hicho huku akijua kwamba yeye ni mjumbe mwenye maslahi na upande mmoja (AZAM FC).
(b) Mchezaji anayetuhumiwa (Juma Said Nyoso) hakupewa nafasi ya kusikilizwa na kamati kama misingi ya utendaji haki inavyohitaji (Principle of natural justice), Klabu inaona mchakato mzima wa usikilizaji wa shauri hili umeingia dosari hivyo maamuzi na adhabu iliyotolewa inakosa sifa kisheria.
3 Mazingira ya tukio lenyewe:
(a) Klabu inatilia shaka ushahidi uliotumika na kutafsiriwa na kamati kufanya uamuzi uliotolewa,kuna uwezekano mkubwa kuwa kamati iliangalia picha ya mnato(Still Picture)iliyosambaa punde baada ya mchezo huo na kuzua mjadala miongoni mwa jamii bila kuangalia mazingira mengine ya tukio hilo.
(b) Katika kipande cha picha mwendo(Video) kinachoonesha chanzo cha tukio hilo ni baada ya mchezaji wa Azam Fc mwenye jezi namba 20 iliyoandikwa Mudathir kumfanyia madhambi mchezaji wa Mbeya City mwenye jezi namba 10,hii ilikuwa faulo yake ya tatu kwa mchezaji huyohuyo bila kuonywa na mwamuzi,Juma Said Nyoso akiwa kiongozi wa wachezaji wa Mbeya City alimfuata Mwamuzi wa mchezo huo kumueleza kuwa Mudathir amekuwa akimchezea sivyo mchezaji huyo bila kuonywa,ndipo John Bocco alipofika eneo ambalo alikuwepo Mwamuzi,Juma Said Nyoso na mchezaji Mwingine wa Mbeya City Fc aliyevaa jezi namba 15 (Christian Sembuli),John Bocco alimpiga kibao usoni Christian Sembuli(Jezi 15) mbele ya muamuzi, wakati John Bocco akifanya hivyo Mudathir(Jezi 20)alizunguka mgongoni kwa John Bocco na kumvuta sehemu za siri(korodani) za Juma Said Nyoso na akarudi upande wa kulia kwa mwamuzi, wakati Mudathir (20) akifanya hivyo John Bocco alimkanyaga na kumpiga teke Juma Said Nyoso.
Klabu inaamini wanaopaswa kuathibiwa ni wachezaji wa AZam Fc John Bocco na Mudathir(20) waliotengeneza mazingira ya kuharibu taswira ya mchezo wa mpira wa miguu mbele ya macho ya watu waungwana.
Mapungufu ya Jumla ya adhabu iliyotolewa:
1. Kamati badala ya kutumia Kanuni ya 37.7(F) ambayo haikatiwi Rufaa wakaitumia Kanuni ya 37(24) ambayo inakatiwa Rufaa.
2. Kamati hawakumpa nafasi ya kujitetea mchezaji husika kwa mujibu wa kanuni ya 37(24).
3. Mwenyekiti wa kamati hii ni Ndugu Said Mohamed ambaye ni Mwenyekiti wa Azam Fc hakusitahili kuongoza wala kuwemo katika kikao hicho kwa kuwa alikuwa na maslahi na timu ya Azam Fc ambao ndio walio mlalamikia mchezaji Juma Said Nyoso.
Umma wa wanamichezo ujifunze nini kutokana na suala hili?
1. Mamlaka zinazosimamia mchezo wa mpira wa miguu ni vizuri sasa kutafsiri kwa upana dhana ya “udhalilishaji” katika mpira wa miguu.
Hii inatokana na namna ambavyo suala hili limeripotiwa na wadau mbalimbali wa mpira wa miguu na wanaharakati,picha za tukio hilo zilisambaa kila uchao.
Klabu inaamini kwa namna wadau walivyolijadili na kulichambua suala hili, lilimdhalilisha zaidi muhusika,kuwekwe utaratibu na chombo ambacho kipewe jukumu la kupitia mashauri na ushahidi wa matukio yanayotafsiriwa kuwa ni ya “udhalilishaji” ili kuendelea kulinda heshima za wahusika katika jamii.
Klabu imewasilisha Tff maelezo ya kutoridhishwa na adhabu aliyopewa Juma Said Nyoso,".

(Imetolewa na E. E. Kimbe, Katibu wa Mbeya City,2/10/2015)

No comments:

Post a Comment