Saturday, October 3, 2015

Stars kucheza Chalenji, waanza kuipashia moto Malawi


TIMU ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) imethibitisha kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge itakayofanyika nchini Ethiopia kuanzia Novemba 21 hadi Desemba 6, mwaka huu.
Michuano ya CECAFA Challenge ndio michuano mikongwe zaidi barani Afrika ambapo jumla ya nchi 12 wanachama hushirki michuano hiyo iliyofanyika mara ya mwisho mwaka juzi nchini Kenya na wenyeji kutwaa Ubingwa huo.
Nchi wanachama wa CECAFA ni Tanzania Bara, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Somali, Sudan, Sudan Kusini na Zanzibar.
Katika hatua nyingine, kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager kimeanza mazoezi leo mchana katika uwanja wa Taifa kujiandaa na mchezo dhdi ya Malawi utakaocheza Jumatano Oktoba 7, 2015 kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Stars inayonolewa na kocha mkuu mzawa Charles Mkwasa, akisaidiwa na Hemed Morroco, Peter Manyika na mshauri wa Ufundi Abdallah Kibadeni wameingia kambini jana katika hoteli ya Urban Rose iliyopo Kisutu jijini Dar es salaam.

Wachezaji wote wameripoti kambini isipokuwa wachezaji wa kimataifa wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, Mrisho Ngasa, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaotarajiwa kuungana na wenzao mwishoni mwa wiki baada ya kumaliza michezo inayowakabili wikiendi hii.
Wachezaji waliopo kambini ni magolikipa All Mustafa, Aishi Manula, Said Mohamed, walinzi Juma Abdul, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Haji Mwinyi, Hassan Isihaka, Kelvin Yondani na nahodha Nadir Haroub “Cannavaro”.
Wengine ni viungo Himid Mao, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Said Ndemla, Salum Telela, Deus Kaseke, Saimon Msuva, Farid Musa, washambuliaji John Bocco, Rashid Mandawa na Ibrahim Hajibu.

No comments:

Post a Comment