Saturday, October 10, 2015

Stand United wasema kocha Liewig ni mbishi balaa


WENYEKITI wa klabu ya Stand United, 'Chama la Wana', Amani Vincent amemshutumu kocha Mkuu wa timu hiyo, Mfaransa Patrick Leiwig kwamba hataki ushauri wa viongozi na wasaidizi wake katika benchi la ufundi.
Akizungumzana mtandao huu, Amani amesema kwamba kocha huyo amekuwa akikaidi na kubeza ushauri unaotolewa na viongozi na hivi karibuni 'alitoleana maneno machafu' na Mwenyekiti huyo alipojaribu kumshauri jambo siku ya mchezo wao dhidi ya Mbeya City mjini Shinyanga.

"Kwa kweli huyu kocha sisi hatumuelewi, maana yeye ukitaka kumpa ushauri hataki, anataka yeye afanye anavyotaka, sasa hii inatupa shida kidogo, maana inasababisha tunashindwa kuelewena na makocha wenzake, lakini tutalifanyia kazi,”amesema Amani.
Hivi karibuni Leiwig alipigwa faini ya Sh. Milioni 1 kufuatia kukiuka sheria za mchezo wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya African Sport, ikiwemo kugoma kuzungumza na Waandishi wa Habari.
Tayari Liewig amemaliza adhabu yake baada ya kutokuwa katika benchi la Stand United kwenye mechi mbili, dhidi ya Simba SC Dar es Salaam timu ikifungwa 1-0 na Mbeya City mjini hapa timu ikishinda 1-0.
Liewig aliyeajiriwa Stand United miezi miwili iliyopita, amewahi kufundisha Simba SC mwaka 2013 na huko alifukuzwa kwa tabia kama hizo, kutofuata ushauri wa uongozi.
Uongozi wa Simba SC ulimshauri Liewig asimpange kipa Juma Kaseja katika mechi dhidi ya Yanga SC, lakini akampanga na baada ya timu kufungwa 2-0 katika mechi hiyo ya mwisho ya msimu, wote kocha huyo na kipa huyo hawakuongezewa mikataba.

No comments:

Post a Comment