Wednesday, October 14, 2015

Fiston aivusha Burundi Kombe la Dunia, Chad yaitoa Sierra Leone


TIMU ya taifa ya Chad imefuzu hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Kombe ka Dunia 2018 nchini Urusi.
Chad wamefungwa 2-1 na Sierra Leone ugenini jana, lakini wanafuzu kwa faida ya bao ya bao la ugenini baada ya sare ya jumla ya 2-2, kufuatia wao kushinda 1-0 nyumbani katika mchezo wa kwanza.
Ikumbukwe Chad ni wapinzani wa Tanzania katika Kundi G kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Gabon. 
Chad itamenyana na Tanzania Machi 25, mwaka huu katika mchezo wa Kundi G kuwania tiketi ya fainali za Mataifa ya Afrika, siku ambayo timu nyingine za kundi hilo, Misri na Nigeria zitakuwa zikimenyana pia kabla ya kurudiana siku tatu baadaye.
Mshambuliaji Fiston Abdul Razak amefunga mabao yote jana Burundi ikishinda 2-0 na kusonga mbele

Mchezo mwingine, mabao mawili ya Fiston Abdul Razak yameisaidia Burundi kushinda 2-0 dhidi ya Shelisheli mjini Bujumbura katika mchezo wa marudiano na kusonga mbele.
Mshambuliaji huyo wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini alifunga dakika ya 68 na 80 na kuivusha Burundi hatua ya mwisho ya mchujo kwa ushindi wa jumla wa 3-0 baada ya kushinda 1-0 katika mchezo wa kwanza.
Botswana imeshinda 3-1 dhidi ya Eritrea jana Uwanja wa Francistown hivyo kufuzu kwa ushindi wa jumla wa 5-1 baada ya awali kushinda 2-1 ugenini.
Mauritania imeifunga 4-0 Sudan Kusini hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 5-1 baada ya sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza.
Liberia imeshinda 3-1 ugenini jana dhidi ya Guinea-Bissau, hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 4-2 baada ya sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza.
Niger imeifumua 4-0 Somalia hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 6-0 baada ya kushinda 2-0 katika mchezo wa kwanza, Namibia imeshinda 2-1 dhidi ya Gambia hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza.
Madagascar imelazimishwa sare ya 2-2 Jamhuri ya Afrika ya Kati, hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 5-2 baada ya kushinda 3-0 katika mchezo wa kwanza ugenini.
Mechi nyingine za marudiano zilichezwa Jumapili na Ethiopia iliifunga 3-0 Sao Tome hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-1 baada ya kuchapwa 1-0 katika mchezo wa kwanza, Kenya ililazimishwa sare ya 0-0 na Mauritius, lakini ikasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 5-2 wa mechi ya kwanza, wakati Tanzania ilifungwa 1-0 na Malawi, lakini ikanufaika na ushindi wa mchezo wa kwanza wa 2-0.

No comments:

Post a Comment