Saturday, October 17, 2015

Hii ndio mikasa inayomkabili maisha ya mkali wa NBA

Lamar Odom 
Kama wewe ni mpenzi wa michezo hususan basketball au kama ni mfuatiliaji wa burudani hasa linapokuja suala la familia maarufu nchini Marekani ya Kim Kardashian basi jina la Lamar Joseph Odom haliwezi kuwa geni masikioni mwako kama si machoni mwako.
Huyu ni mcheaji maarufu wa kikapu akiwa amewahi kuvichezea vilabu vya LA Clippers, Miami Hit, LA Lakers ambako alishinda vikombe viwili vya NBA na tuzo ya mchezaji bora wa ziada wa mwaka maafuru kama ‘six man of the year’.
Umaarufu zaidi aliupata baada ya kuwaoa watoto wa moja ya familia ‘The Kardashian’ mdogowake Kim anayefahamika kwa jina la Khloe Kardashian
Jina la Lamar kwa sasa limetawala vichwa vya habari kunako vyombo vya habari mbalimbali lakini safari hii ikiwa ni katika namna tofauti na yenye kutia majonzi baada ya siku ya juzi kukutwa akiwa hajitambui katika danguro nchini Marekani linalofahamika kama Love Ranch lililopo katika jimbo la Crystal, Nevada nchini Marekani.
Taarifa ya awali aliitoa mmiliki wa danguro hilo Bw. Dennis Hof kuwa Lamar alikuwa hapo kustarehe kwa ajili ya weekend na hakuonekana kutumia madawa ya kulevya ya aina yoyote bali alitumia kwa kiasi kikubwa madawa ya kuongeza nguvu za kiume herbal-viagra ambapo alikuwa akitapika na kutokwa na majimaji yenye rangi kupita pua zake.
Ripoti za awali za kitabibu zinasema kuwa, Lamar alitumia madawa ya kulevya ambayo yalizidi kiwango na sasa anaweza kuwa kaathirika ubongo au kupooza.
Mtaonda huu unakuletea mikasa nyuma ya maisha ya Lamar Odom ambayo pengine ndiyo imeathiri maisha yake kwa kiasi kikubwa na kumfanya kuwa mwanadamu wa tofauti katika kupenda kujihusisha na tabia hatarishi pamoja na muda mwingi kusifika kuwa na hulka za upendo wa hali ya juu na kusaidia wale wanao mzunguka.
Baba yake anafahamika kwa jina la Joe Odom alikimbia familia yake Lamar akiwa mdogo ikiwa ni kutokana na kuathirika na umiaji uliokithiri wa  madawa ya kulevya.
Akiwa na miaka 12 Lamar alifiwa na mama yake mzazi kwa ugonjwa wa saratani, bibi yake ilibidi achukue majukumu ya kumkuza na kufanikiwa kumfikisha katika ligi ya kikapu Marekani NBA mwaka 1999.
Lakini mwaka 2003 miaka minne baada ya kuingia katia NBA bibi yake naye alifariki huku Lamar akiwa na miaka 23 na miaka mitatu baadae mwanye mchanga Jayden Odom alifariki akiwa na miezi sita na nusu akiwa kalala kwenye kitanda maalumu cha watoto.
Katika kuwaweka watu hawa karibu yake japo hawakuwepo tena duniani, Lamar alivaa jezi namba 7 ikiwa ni namba aliyoambiwa na bibi yake kuwa ndiyo namba yake ya bahati. Ikumbukwe miongoni mwa watu aliowapenda zaidi maishani mwake  ni bibi yake mama yake na bibi yake.
Pia alijichora picha ya mama yake mgongoni na katika kifua chake upande wa moyo, alijichora tattoo yenye jina la motto wake Jayden na kabla ya kila mchezo aliandika majina yao kwenye viatu vyake.
Mpaka kufikia kipindi hiki Odom alisimamia majukumu ya mengi yaliyokuwa chini ya bibi yake.
Mwaka 2001 binamu yake alifariki kwa kupigwa risasi na baada ya kutoka msibani, alisababisha ajali iliyopelekea kifo cha kijana mwenye miaka 14, akinukuliwa na jarida la Times alisema: “Kitendo cha kuona binamu yangu akifa na kuona motto akifa pia nilivunjika moyo, nilipata udhaifu mkubwa wa kibinadamu na ikafika hatua nahisi akili yangu haipo sawavifo vimekuwa sehemu yangu, vifo vimekuwa vikinizunguka, nimekuwa nikizika watu na ndugu zangu kwa muda mrefu”.
Masaibu yote haya inasemekana kuchangia kwa kiasi kikubwa yeye kujihusisha na madawa ya kulevya, lakini moja ya vitu vilivyohitimisha safari yake ya mchezo wa kikapu, ni yeye kuachana na mkewake kipenzi Khloe Kardashian.
Katika nyakati tofauti amekiri kumpenda kwa dhati mkewake na kuachana kwao kuliathiri sana maisha ya Lamar. Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida na inayoonesha kwa kiasi gani Lamar amezungukwa na mikasa inayohusisha utumiaji wa madawa, rafiki yake kipenzi na ambaye alisimamia ndoa yake na Khloe alifariki kutokana  na ugonjwa wa unaosababishwa na utumiaji uliokithiri wa madawa ya kulevya.
Mtandao huu unaungana na wanamichezo na watu wote duniani kumuombea Lamar Odom aweze kupona kwa haraka na kurudi katika hali yake ya kawaida .

No comments:

Post a Comment