Wednesday, October 28, 2015

Hans Poppe afunguka kuhusu 'hirizi ya Pape N'Daw


Pape N'daw 
Wenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba Zacharia Hans Poppe ameamua kufunguka juu ya mchezaji raia wa Senegal, Pape Abdoulaye N’daw ambaye amekuwa na vituko katika siku za hivi karibuni, miongoni mwa matukio yake ya kukumbukwa ni pamoja na kuingia uwanjani akiwa amevaa viatu vibovu wakati Simba ilipocheza na Yanga.
Lakini kimbwanga kingine ilikuwa ni kutuhumiwa kuwa na hirizi kwenye mechi iliyopita wakati Simba ilipolala kwa goli 1-0 mbele ya Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
“Unajua wachezaji wengi wanakuwa na vituko mbalimbali lakini pia waandishi wa habari sasahivi naona wamekuwa wanaropoka-ropoka sana kwasababu huyo N’daw hakuwa na hirizi yoyote ila alikuwa amevaa ‘vest’ flan ndani ambayo ni nyeusi”, amesema Poppe.
Pape Nd'aw
“Alikwenda kukaguliwa na kamisaa na akarudi uwanjani, sasa watu wanaandika kwenye magazeti bila hata kuwa na uhakika hata kusubiri ripoti ya kaimisaa na mwamuzi inasemaje. Hakuwa na hirizi, alikuwa amevaa tu nguo tofauti kidogo na wachezaji wa Prisons walikuwa wanafikiria anahirizi”.
“Unajua kwenye mpira wanasema usivae kitu ambacho kitakuwa hatarishi kwa wenzio, na hakuwa na kitu chochote zaidi ya nguo ya kawaida”.

Rekodi zilizowekwa kwenye Ligi mbalimbali Ulaya mwishoni mwa wiki



MUNICH, Ujerumani
NCHINI Ujerumani, klabu ya Bayern Munich ilipata ushindi wake wa 1000 tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo ya Bundesliga baada ya kuifunga FC Koln kwa mabao 4-0.
Katika mchezo huo, golikipa wa Bayern Munich, Manuel Neur aliweka rekodi ya kucheza mchezo wa 138 bila bila kuruhusu wavu wake kutikiswa.
Mchezaji mwingine wa klabu hiyo Arjen Roben aliweka rekodi ya kufunga bao lake la 75 katika ligi ya Bundesliga.
Mshambuliaji wa klabu ya Borussia Dortmund, Pierre Emerick amekuwa mchezaji pekee kutoka klabu ya Dortmund kufunga magoli 13 kwenye mechi 10 ndani ya ligi ya Bundesliga baada ya kufunga magoli matatu (hat-trick) katika ushindi wa Dortmund wa goli 5-1 ilipocheza dhidi ya FC Augsburg.

ITALIA
Klabu ya AS Roma imekwea kileleni mwa Serie A baada ya kupata ushindi wa magoli 2-0 na hiyo inakuwa mara ya kwanza kwa klabu hiyo kukaa kileleni tangu ilipofanya hivyo kwa mara ya mwisho kwenye msimu wa 2013-2014.
Kipa wa AC Milan, Gianluig Donnarumma ameweka rekodi ya kuwa kipa mdogo kucheza mchezo wa Serie A wakati timu yake ilipopata ushindi wa goli 2-1 dhidi ya Sousoro. Bonaroma alidaka kwenye mechi hiyo akiwa na umri wa miaka 16 miezi 8 na siku 6.

UFARANSA
PSG wameendeleza ushindi baada ya ushindi wa goli 4-1 dhidi ya ASSE na kuendelea kukaa kileleni mwa ligi ya Ufaransa.
Mpaka sasa PSG hawajapoteza hata mchezo mmoja kwenye ligi hiyo msimu huu huku timu hiyo ikiwa haijaungwa tangu mwezi Machi mwaka huu tangu walipofungwa na Bodeaux goli 3-2.
Klabu ya Olympic Marseille imepata ushindi wa kwanza kwenye Ligue 1baada ya michezo saba kufuatia ushindi dhidi ya klabu ya Lille wa goli 2-1.

HISPANIA
Baada ya kumshuhudia, Luis Suarez akifunga magoli matatu kwenye ushindi wa goli 3-1 dhidi ya Eibar, kocha wa Barcelona, Luis Enrique Martínez amesema hakuna wa kuziba nafasi ya Suarez hivi sasa.
Ilikuwa ni siku nzuri kwa Suarez kwani alikua akitimiza mwaka mmoja tangu acheze mchezo wake wa kwanza dhidi ya Real Madrid Oktoba 25 2014 katika uwanja wa Santiago Bernabeu.
Hiyo ilikuwa ni hat-trick ya pili kwa Suarez wakati hat-trick ya kwanza ilikuwa ni dhidi ya Cordoba katika ushindi wa Barcelona wa magoli 8-0 msimu uliopita.

ENGLAND
Jurgen Klopp alikuwa akiiongoza Liverpool kwenye mchezo wa kwanza wa ligi ya England katika uwanja wa Unfield dhidi ya Southampton, katika mchezo huo timu hizo zilitoka sare ya kufungana goli 1-1.
Liverpool imefunga magoli tisa tu msimu huu ikiwa timu ya tatu kwa kufunga magoli machache msimu huu ikizizidi klabu za West Brom na Watford pekee ambazo zimefunga magoli nane.
Klabu ya Sunderland imefunga maoli matatu kwa mara ya kwanza tangu tarehe 3 Novemba, 2014. Sunderland iliifunga Newcastle United kwa goli 3-0.
Goli la sekunde ya 49 lililofungwa na Matt Ritchie katika mchezo kati ya Bournemouth dhidi ya Tottenham linakuwa goli la mapema zaidi kwenye msimu wa ligi kuu England. Katika mchezo huo Bournemouth walifungwa goli 5-1 wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Harry Kane alifunga hat-trick yake ya pili kwenye Ligi Kuu England, alifanya hivyo dhidi ya Leicester City msimu uliopita.

Ratiba Ligi Kuu Tanzania Bara



Oktoba 28, 2015
Toto African Vs Mgambo Shooting
Mwadui FC Vs Yanga SC
Mtibwa Sugar Vs Kagera Sugar
Mbeya City Vs Majimaji FC
Ndanda FC Vs Stand United
Simba SC Vs Coastal Union
Oktoba 29, 2015
JKT Ruvu Vs Azam FC 
Prisons Vs African Sports

MCHEZAJI bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwezi Septemba, Hamisi Friday Kizza ‘Diego’ yuko tayari kurudi uwanjani leo.
Mganda huyo hajaonekana uwanjani tangu Simba SC ifungwe 2-0 na mahasimu, Yanga SC, Septemba 26, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini leo anaweza kurudi.
Simba SC inamenyana na Coastal Union ya Tanga katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo Uwanja wa Taifa na Ofisa Habari wa Simba SC, Hajji Sunday Manara amesema Kizza anaweza kurudi.
“Kama mchezaji yuko fiti na amefanya mazoezi kikamilifu kuelekea mchezo huu, sasa ni jukumu la kocha mwenyewe kumuanzisha au la. Maana kocha wetu (Muingereza Dylan Kerr) naye ana maamuzi yake,”amesema.
Mbali na Kizza, Manara amesema hata kiungo wao, Jonas Mkude naye yuko vizuri kabisa kuelekea mchezo wa leo na wanamuachia Kerr mwenyewe kama kawaida yake aamue wachezaji wa kutumia.
Kwa ujumla Manara amesema Simba SC haina mchezaji majeruhi wala mgonjwa kuelekea mchezo wa leo na wanasubiri kuona kocha Kerr atawapangia timu ya aina gani leo.
Kwa ujumla, Ligi Kuu inaendelea leo, mbali na Simba na Coastal- Mwadui FC inaikaribisha Yanga SC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Toto Africans watakuwa wenyeji wa Mgambo Shooting Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa ndugu zao Kagera Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro. 
Mbeya City watakuwa wenyeji wa Majimaji FC Uwanja wa Sokoine, Ndanda FC wataikaribisha Stand United Uwanja wa Nangwanda, Mtwara wakati kesho JKT Ruvu watamenyana na Azam FC Uwanja wa Karume, Dar es Salaam na Prisons wataikaribisha African Sports Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Thierry Henry amtaja mchezaji Ligi Kuu England

Scholes 1
Gwiji la soka na mchezaji wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry amewashangaza wengi kwa kumtaja kiungo wa zamani wa England na Manchester United, Paul Scholes kuwa ndiye bora amewahi kukutana naye katika historia ya premier league.
Akijibu swali katika interview moja na Sky Sport, alipotakiwa kumtaja mchezaji bora wa muda wote wa ligi kuu England, tofauti na mashabiki wengi ambao wamekua wakiwapa vipaumbele akina Shearer, Henry mwenyewe, Giggs na Cristiano Ronaldo, lakini nahodha huyo wa zamani wa Arsenal amemtaja Paul Scholes kuwa hana mfano wake.
Scholes
Henry anasema Paul Scholes ndiye mchezaji pekee aliyeweza kuufanya mpira chochote na kwamba kwa mujibu wa Henry, Scholes amekua hapati heshima na sifa anazostahili.
“Paul Scholes ni bora zaidi mimi kuwahi kukutana naye. Timu ya taifa haikutambua ubora wake, lakini Manchester United waliutumia uwezo wake vizuri”.
Scholes 2
Xavi Hernandez wa Barcelona anatajwa kuwa ndiye kiungo bora zaidi kwa miaka kumi, aliwahi kusema kuwa kama yeye ni bora kwa miaka kumi, basi Scholes ni kwa miaka 20.
Scholes 3
Xavi anasema alikua akiongea na Alonso mara nyingi na kwamba Paul Scholes ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi wa kizazi chake. Xavi anasema Scholes anaweza kupiga pasi za goli, ndefu na fupi huku akiwa na uwezo mkubwa sana wa ku-control temper ya mchezo.
SPT-GCK-210604- Euro 2004 Portugal England V Croatia Picture Graham Chadwick Scholes goal


Matokeo yote ya mechi za Capital One

Capital One Cup 1
Usiku wa Jumanne nchini England kulipingwa michezo minne ya kombe la Capital One, michezo mitatu kati ya minne iliamuliwa kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya michezo yote mitatu kumalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1.
Sheffield Wednesday wakapata ushindi wa goli 3-0 mbele ya Arsenal na kuing’oa Arsenal kwenye kombe la kwanza msimu huu.
Chelsea dhidi ya Stoke Cty mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Britania Stoke ikafanikiwa kuivua ubingwa Chelsea baada ya kuifunga kwa mikwaju ya penati 5-4 kufuatia sare ya kufungana goli 1-1. Walters aliifungia Stoke City goli la kuongoza dakika ya 52 lakini Loic Remy akaisawazishia Chelsea dakika ya 90.
Eden Hazard akakosa mkwaju wa penati wa mwisho baada ya dakika 120 za mchezo na kuhitimisha safari ya Chelsea kwenye michuano ya Capita One Cup.
Hull City waliwakaribisha Leicester City, Abel Hernandez aliifungia Hull City bao lakini  Riyad Mahrez akaifungia Leicester City bao la kusawazisha na kuufanya mchezo huo kuchezwa kwa dakika 120 na kumalizika kwa matokeo hayo ya kufungana bao 1-1.
Kwenye changamoto ya mikwaju ya penati, Hull City wakafanikiwa kusonga mbele baada ya Riyad Mahrez kukosa penati yake.
Kwenye uwanja wa Goodson Park Everton waliwakaribisha Norwich City mchezo uliomalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1. Zikaongezwa dakika 30 lakini bado timu hizo hazikufuyngana, ikabidi itumike mikwaju ya penati kumpata mshindi na Everton wakafanikiwa kusonga mbele.
Capital One Cup results


Fifa yathibitisha majina saba ya wagombea urais

FIFA
Shirikisho la soka dunia FIFA limetoa orodha ya wagombea wa kinyang’aniro cha Urais wa shrikisho hilo katika uchaguzi utakaofanyika tarehe ya 26 mwezi wa pili 2016.
Katika majina hayo wamo Prince Ali Bin Hussein wa Jordan,Musa Bility wa Liberia,mkurugenzi wa zamani wa masuala ya uhusiano wa kimataifa wa FIFA Jerome Champagne toka nchini Ufaransa,Katibu mkuu wa UEFA Gianni Infantino raia wa Uswisi,Rais wa UEFA Michel Platini , Sheikh Salman Bin Ebrahim Al Khalifa wa Bahrain na Mosima Gabriel maarufu kama ‘Tokyo Sexwale’ wa Afrika Kusini.
Rais wa Shirikisho la soka barani Ulaya ataendelea kuwepo katika kinyang’anyiro hicho mpaka hapo kamati ya maadili ya FIFA itakapotolea majibu ya rufaa ya kiongozi huyo wa soka barani Ulaya.
Lakini kamati ya uchaguzi wa FIFA imesema kuwa haitomweka katika kinyang’anyiro cha Urais Michel Platini mpaka adhabu yake itakapotenguliwa na kamati ya maadili ya FIFA.
Kwa sasa Michel Platini amefungiwa kutojihusisha na soka kwa muda wa siku 90.

Algeria yaweka kikosi hadharani cha kuivaa Stars


Algeria
Algeria tayari imetangaza kikosi cha awali cha wachezaji 32 kitakachoivaa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia zitakazofanyika mwaka 2018 nchini Urusi.
Stars na Algeria zitachuana Novemba 14 mwaka huu kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam ukiwa ni mchezo wa kwanza kabla ya kurudiana siku tatu baadae nchini Algeria.
Kuelekea mchezo, Algeria ‘Mbweha wa Jangwani’ imewaita wachezaji wake wengi wanaocheza soka la kulipwa kwenye vilabu vya Ulaya ikiwa ni pamoja na kiungo kinda Bentaleb anayekipika kwenye klabu ya Tottenham, Marhez Riyad na Adlane Guedioura wanaocheza kwenye vilabu vya Leicester na Watford vya England.
Wengine waliojumuishwa kwenye kikosi hicho ni pamoja na Brahimi Yassine (Porto), Sofiane Feghouli (Valencia), Slimani Islam (Sporting Lisbon), Abeid Mehdi (Panathinaicos), Ryad Boudebouz (Montpellier), Saphir Taider (Bologna) na Zeffane Mehdi (Rennes).
Wengine Benrhama Said (Nice), Soudani Hilal Al Arabi (Dinamo Zagreb), Mesbah Djamel Eddine ni (Sampdoria), Rachid Ghezzal (Lyon) and Walid Mesloub (Lorient).
Taifa Stars ilifuzu kucheza raundi ya pili baada ya kuiondosha Malawi kwa wastani wa goli 2-1 kwenye raundi ya awali ya kuwania kufuzu kucheza michuano ya kombe la dunia kufuatia ushindi wa nyumbani wa Stars wa goli 2-0 huku ikipoteza mchezo wake wa ugenini (Malawi) kwa goli 1-0.

Wednesday, October 21, 2015

Mechi za Simba, Azam yaahirisha kupisha maandalizi ya Stars na Algeria

MECHI za raundi ya 11 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zilizokuwa zichezwe Novemba 7 na 8 mwaka huu sasa zitafanyika Desemba 12 na 13 kupisha maandalizi ya Taifa Stars ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia.
Taifa Stars inatarajia kuingia kambini mapema mwezi ujao kujiandaa na mechi ya kwanza dhidi ya Algeria ambayo itafanyika Novemba 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zitarudiana nchini Algeria, Novemba 17 mwaka huu.
Mechi hizo za Vodacom zitakazochezwa Desemba 12 ni kati ya Mgambo Shooting na Yanga (Tanga), Kagera Sugar na Ndanda (Tabora), Stand United na Mwadui (Shinyanga), Mbeya City na Mtibwa Sugar (Mbeya), Azam na Simba (Dar es Salaam) na Majimaji na Toto Africans (Songea). Mechi za Desemba 13 ni kati ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons (Dar es Salaam), na Coastal Union na African Sports (Tanga).
Pia mechi tatu za raundi ya sita ambazo hazikuchezwa Oktoba 4 mwaka huu kupisha mechi ya Taifa Stars na Malawi sasa zitafanyika Desemba 16 mwaka huu. Mechi hizo ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar (Dar es Salaam), na African Sports na Yanga (Tanga), mchezo kati ya Ndanda na Simba (Mtwara utapangiwa tarehe ya kuchezwa.
Nayo mechi namba 59 kati ya JKT Ruvu na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe Oktoba 21 mwaka huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam imesogezwa mbele kwa siku moja hadi Oktoba 22 mwaka huu ili kuipa nafasi ya mapumziko JKT Ruvu ambayo jana (Oktoba 18 mwaka huu) ilicheza mechi yake ya raundi saba mkoani Shinyanga.

Gharama za kiingilio chaikwamisha Wajerumani

Mashabiki wa Bayern Munich wakiwa wamebabeba mabango yenye ujumbe wa kupinga bei za viingilio vikubwa kwenye uwanja wa Emirates
Mashabiki wa Bayern Munich wakiwa wamebabeba mabango yenye ujumbe wa kupinga bei za viingilio vikubwa kwenye uwanja wa Emirates
Uwanja wa Emirates unaomilikiwa na Arsenal ndio unaoongoza kwa tozo kubwa ya viingilio vyake jijini London. Katika mchezo huo kati ya Arsenal na Bayern Munich, baadhi ya mashabiki wa Bayern walikataa kuingia uwanjani kutokana na bei kubwa za kiingilio.
Kikundi hicho cha mashabiki kutoka Ujerumani walikaa nje kwa dakika tano kabla ya kukubali kuingia uwanjani na kupata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki wa Arsenal walipokua wakiketi katika seat zao.
Mashabiki hao waliingia na mabango waliyoyaandika, “tiketi paun 64?… Hakuna soka bila ya mashabiki”. Ujumbe huo uliandikwa kuonesha kutokukubaliana na gharama za uwanja huo.
Mashabiki wa Arsenal wakiwashangilia mashabiki wa Bayern Munich baada ya kukubali kuingia uwanjani kufuatia kugoma kwa dakika kadhaa
Mashabiki wa Arsenal wakiwashangilia mashabiki wa Bayern Munich baada ya kukubali kuingia uwanjani kufuatia kugoma kwa dakika kadhaa
Kocha wa Bayern Munich, Pep Guadiola alisema ataongea na Arsene Wenger siku nyingine wajaribu kuweka bei nafuu za viingilio kuwapa nafasi mashabiki wote kuingia uwanjani. Guadiola amesema kwa upande wake yeye Ujerumani atawajali mashabiki wa Arsenal na kuhakikisha wanapata viingilio rahisi washuhudie mechi.
Aidha katika mchezo wenyewe, Arsenal walifanikiwa kushinda kwa magoli 2-0 mbele ya Bayern Munich na kupata ushindi wa kwanza kabisa tangu kuanza kwa michuano hiyo ya Ulaya msimu huu.

Matokeo ya mechi zote za Ligi ya mabingwa Ulaya

Dynamo Kiev vs Chelsea 
Usiku wa Jumanne imepigwa michezo kadhaa ya vilabu bingwa barani Ulaya maarufu kama UEFA Champions League na kushuhudia matokeo tofautitofauti kwenye viwanja mbalimbali.
Hapa nimekuletea matokeo ya timu zote ambazo zilijitupa uwanjani kusaka pointi muimu kwa ajili ya kujiweka vizuri kwa ajili ya kufuzu kwenye hatua inayofutata ukiachilia mbali hatua ya makundi.
UEFA Matokeo 20 Oct

Stand United yaitisha mkutano mkuu wa dharura

Kikosi cha Stand United
Kikosi cha Stand United
 Klabu ya Stand United imeandika barua ya kuitisha mkutano mkuu wa dharura utakaofanyika Octoba 30, 2015 wenye lengo la kupitisha katiba mpya ya klabu hiyo.
Barua hiyo imeandikwa kwa katibu mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania kuomba kupewa mwakilishi toka TFF kwa ajili ya kushuhudia zoezi hilo muhimu.
Hii hapa ni barua ya mwenyekiti wa klabu ya Stand United kwenda kwa katibu mkuu wa TFF.
Barua Stand United
Barua Stand United 1

Cannavaro awachambua Mwambusui, Mkwasa

Nadir Haroub
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amemchambua kocha mpya msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi na kumlinganisha na aliyekuwa kocha msaidizi wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa na kusema wawili hao hawana tofauti kabisa.
Mwambusi alichukua mikoba ya Mkwasa ya kuwa msaidizi wa kocha, Hans Van Pluijm wiki iliyopita baada ya Mkwasa kupewa mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa kuinoa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Cannavaro alisema kuwa katika kipindi alichokaa na Mwambusi amegundua kuwa kocha huyu hapendi utani kwenye suala zima la nidhamu za wachezaji na siku zote amekuwa akisisitizia suala hilo kama ilivyokuwa kwa Mkwasa.
Cannavaro alisema kuwa kutokana na hali hiyo, hivi sasa ana matumaini makubwa sana na timu yao na nidhamu haitakuwa tatizo kwenye kikosi cha Yanga kitu ambacho kitachangia kuwapa ubingwa mapema msimu huu.
“Kwa muda mfupi niliokuwa na Mwambusi baada ya kurejea kutoka Stars nimeona anaweka mbele masuala ya nidhamu na kujituma kuliko kitu chochote na hivi ndivyo alivyokuwa Mkwasa,” alisema Mwambusi.
“Mwambusi ni mtu wa utani sana na tabia yake hii imesababisha wachezaji tumzoee haraka sana na tunaona kama tumekaa naye zaidi ya mwaka, kinachonifurahisha zaidi ni kuwa anapita kwenye njia zile zile za Mkwasa, hii itatusaidia kutupa matokeo bora na inafahamika kuwa ili timu iwe bora lazima nidhamu izingatiwe,” Cannavaro aliiambia Bingwa.
Cannavaro aliwataka pia wachezaji wa kikosi hicho kufanya kazi kiweledi, kujituma na kufuata kila wanaloelekezwa na benchi la ufundi kwani bado wana safari ndefu yenye changamoto kuelekea katika kutetea ubingwa wao.

Coastal Union yamtimua Mayanja

KIKAO cha Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Coastal Union kilichoketi juzi kwa saa tatu kilitoka na mapendekezo wa kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo,Jackson Mayanja kutokana na kutokuwepo kwa mwenendo wa matokeo mazuri kwa timu hiyo tokea alipokabidhiwa. 

Kocha Mayanja alikabidhiwa kikosi hicho cha Wagosi wa Kaya baada ya kumalizika msimu wa ligi kuu uliopita akichukua mikoba ya Jamhuri Kihwelu “Julio” ambaye aliinusuru timu hiyo na kushuka daraja ikimaliza ikiwa nafasi tano za juu kwenye msimamo.
 
Akizungumza mara baada ya kumalizika kikao hicho,Ofisa Habari wa Coastal Union,Oscar Assenga alisema kuwa kikao hicho kilikutana chini ya Mwenyekiti wao Dr.Ahmed Twaha ambapo pamoja na mambo mengine kilikuwa na agenda kadhaa lakini kubwa ikiwa sababu za timu hiyo kutokufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi kuu.
Assenga alisema kuwa agenda hiyo ilikuwa mzito kwa wajumbe kutokana na timu usajili makini uliofanywa kwa wachezaji lakini wakaonekana kushindwa kuendana na kasi iliyokuwa ikitakiwa ili kuweza kuipa mafanikio timu hiyo kwenye mechi zao.
Alisema kuwa sababu kubwa zilizopelekea kuachana na kocha huyo zinatokana na aina ya ufundishaji wake kutokuendana na kasi ya timu hiyo kutokana na wachezaji kukosa stamina hali iliyopelekea kushindwa kucheza kwa mafanikio kwenye mechi zao.
 “Lakini hata ukiangalia wakati wa mazoezi wachezaji wetu wamekuwa wakichezeshwa nusu uwanja huku kwenye mechi za ligi kuu wanatakiwa kucheza uwanja mzima pamoja na timu yetu kupoteza stamina na wachezaji kupoteza umakini kutokana na aina ya ufundishaji wake,”Alisema
Aidha alisema kuwa baada ya mechi ya leo(jana) timu hiyo itakuwa chini  ya Mbwana Bushiri Akisaidiana na Kamati ya Ufundi ya timu hiyo ambao watakuwa na jukumu la kuiandaa timu hiyo kuelekea mapambano ya Ligi kuu soka kwenye mechi zinazofuata.
Hata hivyo alisema kuwa tayari Mwenyekiti wa timu hiyo,amemuagiza Katibu Mkuu wa timu hiyo,Kassim El Siagi kuwaandikia barua Kamati ya Ufundi haraka iwezekanavyo ili waweze kutambua majukumu yao hayo mpaka atakapopatikana Kocha Mpya.

Taarifa mpya kuhusu Nsa Job

Nsa Job, mchezaji wa zamani wa vilabu vya Simba , Yanga na Cosatal Union
Nsa Job, mchezaji wa zamani wa vilabu vya Simba , Yanga na Cosatal Union
Baada ya picha nyingi na taarifa kuzagaa zinazomhusu mchezaji wa zamani wa vilabu vya Yanga, Simba pamoja na Coastal Union Nsa Job akiwa amelazwa hospitali kufuatia kujeruhiwa vibaya na watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa CHADEMA, imetoka taarifa kuwa hali yake inaendelea kuwa nzuri.
Mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Kilimanjaro Goodluck Moshi amesema hali ya Nsa Job anaendelea vizuri akiwa bado amelazwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi lakini tayari ameondolewa mashine za kumsaidia kupumua.
“Taarifa iliyopo ni kwamba, alipigwa (Nsa Job) na jiwe kubwa kichwani wakati akiwa kwenye gari akitokea nyumbani kwa mgombea ubunge Manispaa ya Moshi kupitia Chama Cha Mapinduzi Ndugu Davis Mosha”, Moshi ametaarifu .
“Wakati wanatoka nyumbani kwa Mosha wakiwa kwenye gari yeye (Nsa Job), Mosha na mtu mwingine, walipofika barabarani, likarushwa jiwe kubwa likapita kwenye kioo cha dirisha na kumpasua kwenye kichwa na taya, akakimbizwa KCMC amefanyiwa upasuaji bado yupo ICU lakini hali yake inaendelea vizuri”.
“Ameshaondolewa mashine za kupumulia na anaweza kuongea hivi sasa, ni jambo la kumshukuru Mungu kutokana na hali halisi ilivyokuwa imejitokeza”.
Jana kuna picha zilienea kwenye mitandao ya kijamii zikionesha kuwa Nsa Job amelazwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) baada ya kujeruhiwa vibaya kwenye eleo la kichwa.

Saturday, October 17, 2015

Hii ndio mikasa inayomkabili maisha ya mkali wa NBA

Lamar Odom 
Kama wewe ni mpenzi wa michezo hususan basketball au kama ni mfuatiliaji wa burudani hasa linapokuja suala la familia maarufu nchini Marekani ya Kim Kardashian basi jina la Lamar Joseph Odom haliwezi kuwa geni masikioni mwako kama si machoni mwako.
Huyu ni mcheaji maarufu wa kikapu akiwa amewahi kuvichezea vilabu vya LA Clippers, Miami Hit, LA Lakers ambako alishinda vikombe viwili vya NBA na tuzo ya mchezaji bora wa ziada wa mwaka maafuru kama ‘six man of the year’.
Umaarufu zaidi aliupata baada ya kuwaoa watoto wa moja ya familia ‘The Kardashian’ mdogowake Kim anayefahamika kwa jina la Khloe Kardashian
Jina la Lamar kwa sasa limetawala vichwa vya habari kunako vyombo vya habari mbalimbali lakini safari hii ikiwa ni katika namna tofauti na yenye kutia majonzi baada ya siku ya juzi kukutwa akiwa hajitambui katika danguro nchini Marekani linalofahamika kama Love Ranch lililopo katika jimbo la Crystal, Nevada nchini Marekani.
Taarifa ya awali aliitoa mmiliki wa danguro hilo Bw. Dennis Hof kuwa Lamar alikuwa hapo kustarehe kwa ajili ya weekend na hakuonekana kutumia madawa ya kulevya ya aina yoyote bali alitumia kwa kiasi kikubwa madawa ya kuongeza nguvu za kiume herbal-viagra ambapo alikuwa akitapika na kutokwa na majimaji yenye rangi kupita pua zake.
Ripoti za awali za kitabibu zinasema kuwa, Lamar alitumia madawa ya kulevya ambayo yalizidi kiwango na sasa anaweza kuwa kaathirika ubongo au kupooza.
Mtaonda huu unakuletea mikasa nyuma ya maisha ya Lamar Odom ambayo pengine ndiyo imeathiri maisha yake kwa kiasi kikubwa na kumfanya kuwa mwanadamu wa tofauti katika kupenda kujihusisha na tabia hatarishi pamoja na muda mwingi kusifika kuwa na hulka za upendo wa hali ya juu na kusaidia wale wanao mzunguka.
Baba yake anafahamika kwa jina la Joe Odom alikimbia familia yake Lamar akiwa mdogo ikiwa ni kutokana na kuathirika na umiaji uliokithiri wa  madawa ya kulevya.
Akiwa na miaka 12 Lamar alifiwa na mama yake mzazi kwa ugonjwa wa saratani, bibi yake ilibidi achukue majukumu ya kumkuza na kufanikiwa kumfikisha katika ligi ya kikapu Marekani NBA mwaka 1999.
Lakini mwaka 2003 miaka minne baada ya kuingia katia NBA bibi yake naye alifariki huku Lamar akiwa na miaka 23 na miaka mitatu baadae mwanye mchanga Jayden Odom alifariki akiwa na miezi sita na nusu akiwa kalala kwenye kitanda maalumu cha watoto.
Katika kuwaweka watu hawa karibu yake japo hawakuwepo tena duniani, Lamar alivaa jezi namba 7 ikiwa ni namba aliyoambiwa na bibi yake kuwa ndiyo namba yake ya bahati. Ikumbukwe miongoni mwa watu aliowapenda zaidi maishani mwake  ni bibi yake mama yake na bibi yake.
Pia alijichora picha ya mama yake mgongoni na katika kifua chake upande wa moyo, alijichora tattoo yenye jina la motto wake Jayden na kabla ya kila mchezo aliandika majina yao kwenye viatu vyake.
Mpaka kufikia kipindi hiki Odom alisimamia majukumu ya mengi yaliyokuwa chini ya bibi yake.
Mwaka 2001 binamu yake alifariki kwa kupigwa risasi na baada ya kutoka msibani, alisababisha ajali iliyopelekea kifo cha kijana mwenye miaka 14, akinukuliwa na jarida la Times alisema: “Kitendo cha kuona binamu yangu akifa na kuona motto akifa pia nilivunjika moyo, nilipata udhaifu mkubwa wa kibinadamu na ikafika hatua nahisi akili yangu haipo sawavifo vimekuwa sehemu yangu, vifo vimekuwa vikinizunguka, nimekuwa nikizika watu na ndugu zangu kwa muda mrefu”.
Masaibu yote haya inasemekana kuchangia kwa kiasi kikubwa yeye kujihusisha na madawa ya kulevya, lakini moja ya vitu vilivyohitimisha safari yake ya mchezo wa kikapu, ni yeye kuachana na mkewake kipenzi Khloe Kardashian.
Katika nyakati tofauti amekiri kumpenda kwa dhati mkewake na kuachana kwao kuliathiri sana maisha ya Lamar. Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida na inayoonesha kwa kiasi gani Lamar amezungukwa na mikasa inayohusisha utumiaji wa madawa, rafiki yake kipenzi na ambaye alisimamia ndoa yake na Khloe alifariki kutokana  na ugonjwa wa unaosababishwa na utumiaji uliokithiri wa madawa ya kulevya.
Mtandao huu unaungana na wanamichezo na watu wote duniani kumuombea Lamar Odom aweze kupona kwa haraka na kurudi katika hali yake ya kawaida .

Barcelona kuishangaza dunia kumsajili Robin van Persie

2D70766F00000578-0-image-a-8_1444908771167
Ilionekana kwamba Van Persie yupo kwenye siku zake za mwisho kwenye soka na akahamia club ya Fenerbahce akitokea Manchester united. Sasa habari mpya ni kwamba Van Persie anatakiwa kujiunga na club ya Barcelona ikifika mwezi wa kwanza 2016.
Barcelona wanatafuta foward mwingine atakayekua back up wa wachezaji watatu Neymar, Messi na Suarez. Combination ya hawa watatu imeonekana kulegea baada ya Messi kuwa nje ya uwanja na hakuna mchezaji mwigine anaekamilisha hiyo crew ya wachezaji watatu kama Barcelona ilivyozoea kucheza.
Van Persie ambae yupo Fenerbahce anaweza kuwa nafasi ya kuhamia Barcelona kama inayo ripotiwa sasa hivi kutokana na kutokua na maelewano mazuri na kocha wake. Kutokuelewana huko inatokana na kwasababu Van Persie anatupia mara chache sana nyavuni kama ilivyotegemewa.
Barcelona wanahitaji kuwa na uhakika na kikosi chao kwa sababu wapo kwenye vita ya kutetea makombe makubwa ambayo waliyashinda kwenye msimu uliopita

Martial kweli noma

Anthony Martial-tuzo 
Mshambuliaji wa klabu ya Manchester United Anthony Martial ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Septemba ikiwa ni tuzo ya kwanza kwa mchezaji wa Manchester United kwenye ligi kuu England chini ya kocha Louis van Gaal tangu ajiunge na klabu hiyo mwaka 2014.
Martial amecheza michezo minne kwenye ligi kuu ya England na tayari ameshafunga magoli matatu, Manchester United itacheza na Everton kwenye uwanja wa Goodson Park.
Kinda huyo wa Kifaransa alitua Old Trafford akitokea Monaco kwa ada ya uhamisho wa pauni 36 huku kukiwa na kipengele cha kuongezeka hadi pauni milioni 58.
Martia aliunga goli lake la kwanza dhidi ya Liverpool alipotokea benchi ambapo United iliibuka na ushindi wa goli 3-1. Mchezo kati ya Manchester United dhidi ya Southampton, Martial alifunga mgoli mawili wakati Manchester iliposhinda kwa goli 3-2.
Wakati Martial akichukua tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Septemba, kocha wa Tottenham Mauricio Pochettino amechukua tuzo ya kocha bora wa mwezi wa tisa.

Ukiacha Uholanzi, hizi ni timu nyingine ambazo hazijafuzu

FBL-EURO-2016-NED-CZE 
Usiku Oktoba 13, 2015 ni wa kukumbukwa sana na wapenzi wa soka duniani hasa kwa wale mashabiki wa timu ya taifa ya Uholanzi maarufu kama ‘Orange’.
Timu ya taifa ya Uholanzi imeshindwa kufuzu michuano ya Ulaya baada ya kufungwa na timu ya taifa ya Jamhuri ya watu wa Czech kwa bao 3-2 katika uwanja wa Amsterdam Arena, Uholanzi.
Ilikuwa ni simanzi kubwa sana nchini Uholanzi, kichapo chao kimeifanya timu hiyo ishike nafasi ya nne katika kundi A lililokuwa na timu kama Jamhuri ya watu wa Czech, Island, Uturuki, Kazakhstan, Latvia na Uholanzi yenyewe.
Timu ambazo zimefuzu katika kundi hilo ni Island, Jamhuri ya watu wa Czech na Uturuki. Ni miaka 31 tangu kwa mara ya mwisho Uholanzi kushindwa kufuzu kwenye michuano ya Ulaya ya mwaka 1984 iliyofanyika nchini Ufaransa. Na mwaka huu 2015, Uholanzi imeshindwa kufuzu michuano ya Ulaya itakayofanyika Ufaransa mwaka 2016.
Uholanzi si nchi ya kwanza kushindwa kufuzu michuano mikubwa ya soka duniani, zipo pia nchi nyingine ambazo zimewahi kushindwa kufuzu michuano mbalimbali ya soka angali nchi hizo zikiwa na majina makubwa sana katika mchezo huo.
  ENGLAND
Baada ya kutwaa ubingwa wa dunia mwaka 1966 bado walishindwa kufuzu kucheza michuano ya kombe la dunia ya mwaka 1974 iliyofanyika nchini Ujerumani Magharibi baada ya kushindwa kuifunga timu ya taifa ya Poland katika uwanja wa Wembley.
England walishindwa pia kufuzu michuano ya kombo la dunia mwaka 1978 iliyofanyika nchini Argentina kabla ya kushindwa kufuzu fainali za kombe la dunia fainali za mwaka 1994.
Chini ya kocha Stive McLaren England ilishindwa kufuzu michuano ya Ulaya mwaka 2008 iliyofanyika katiika nchi za Austria na Uswis baada ya kufungwa na Croatia kwa goli 3-2 mwaka 2007.
SCOTLAND
Ikiwa na nyota wengi wa Celtic waliotwaa kombe la washindi barani Ulaya mwaka 1967 ilishindwa kufuzu michuano ya kombe la dunia mwaka 1970 iliyofanyika nchini Mexico. Scoland ilikubali kichapo cha goli 2-0 kutoka kwa Austria uliofanyika mjini Viena na kufuta ndoto za timu hiyo kushiriki michuano ya kombe la dunia.
UHOLANZI
Dunia ilipata mshtuko katika michezo ya kufuzu kucheza michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2002 baada ya timu ya taifa ya Uholanzi kushindwa kufuzu kwenye michuano hiyo iliyoandaliwa kwa pamoja na nchi za Japan na Korea Kusini.
Uholanzi ya wakati huo iliyokuwa na nyota wengi kama Ruud van Nistelrooy, Patrick Kluivert, Edger Davis na wengine chini ya kocha Louis van Gaal. Uholanzi ilishika nafasi ya tatu katika kundi lake nyuma ya Jamhuri ya watu wa Ireland ambao waliongoza kundi.
URENO
Mkasa wa kushindwa kufuzu kwenye michuano mikubwa pia umeikumba timu ya Ureno, timu hiyo iliyokuwa na kikosi cha dhahabu wakati huo miaka ya 1990 mpaka 2000 ilishindwa kufuzu michuano ya kombe la dunia iliyofanyika nchini Ufaransa mwaka 1998.
Nyota wa Ureno wa wakati huo alikuwa ni Louis Figo na wengineo walishindwa kuipeleka nchi yao katika fainali za kombe la dunia nchini Ufaransa.
UFARANSA
Ufaransa nao wapo katika kundi hilo kwa kukosa michuano ya kombe la dunia baada ya kukosa kushiriki fainali za mwaka 1994 zilizofanyika Marekani. Ikiwa na nyota kama Didier Deschamps (kocha wa sasa wa timu ya taifa ya Ufaransa), na Eric Cantona ilihitaji pointi moja tu katika michezo miwili dhidi ya Bulgaria na Israel.
Chakushangaza ni kwamba, Ufaransa ilipoteza michezo yake yote na kushindwa kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 1994.

Nani kumvaa nani kuwania kombe la Dunia

HATUA ya mwisho ya mchujo wa kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi kwa kanda ya Afrika inatarajiwa kufanyika katikati ya Novemba.
Mechi mbili zitachezwa, moja nyumbani na nyingine ugenini na washindi wa jumla wataingia kwenye makundi matano, ambayo mwishowe kila kundi litatoa timu moja ya kwenda Urusi mwaka 2018.
Mshambuliaji wa Azam FC, Alan Wanga aliisaidia Kenya kufuzu hatua ya mwisho ya mchujo Kombe la Dunia na sasa itamenyana na Carpe Verde

RATIBA YA HATUA YA MWISHO KOMBE LA DUNIA
Niger v Cameroon
Mauritania v Tunisia
Namibia v Guinea
Ethiopia v Kongo
Chad v Misri
Comoros v Ghana
Swaziland v Nigeria
Botswana v Mali
Burundi v DRC
Liberia v Ivory Coast
Madagascar v Senegal
Kenya v Cape Verde
Tanzania v Algeria
Sudan v Zambia
Libya v Rwanda
Morocco v Equatorial Guinea
Msumbiji v Gabon
Benin v Burkina Faso
Togo v Uganda
Angola v Afrika Kusini

Simba walia kuwa TFF imejaa Uyanga

KLABU ya Simba SC imelalamika kwamba, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) haliwatendei haki kwa sababu uongozi wake umesheheni watu wa Yanga SC.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba, imefikia TFF wamekata kabisa mawasiliano na klabu yao.
Poppe amesema kwamba TFF sasa hawajibu hata barua za Simba SC wanapoandika kuhoji au kuomba ufafanuzi wa jambo lolote.
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema kwamba imefikia wakati wanashindwa hata kujua namna gani wanaweza kupata haki zao nyingine za msingi, kutokana na ‘kuchuniwa’ na TFF.
“Inafahamika kwamba Rais wa TFF (Jamal Malinzi), Katibu wake (Mwesigwa Selestine) wote ni Makatibu wa zamani wa mahasimu wetu, Yanga SC. Na bado wapo wengine wengi pale TFF ambao wametoka Yanga akina Baraka Kizuguto.
“Lakini kwa sababu wanaongoza chombo cha kitaifa, wanapaswa kutenda haki, yaani inaonekana kabisa TFF wanaikandamiza Simba na wanaibebea Yanga,”amelalamika Poppe.
Akifafanua, mfanyabiashara huyo maarufu nchini, amesema TFF hawajajibu barua yoyote ya Simba SC kwa mwaka huu na hawaelewei sababu ni nini.
“Watuonyeshe wao, ni barya ipi ya Simba SC wamejibu mwaka huu, malalamiko yetu ya mchezo dhidi Yanga hawakujibu, Suala la Messi (Ramadhani Singano) hawakujibu. Hata tunapojibu barua zao za adhabu wanazotuandika ili kuomba ufafanuzi, pia hawatujibu. 
“Labda watuambie basi kwamba barua zetu tunatakiwa kuzipitishia Yanga SC ndiyo watujibu, tutafanya hivyo, tutaandika na kuwapelekea Yanga waweke muhuri wao ipelekwe TFF, tujibiwe, hiyo ndiyo shida yetu,”amesema.
Hans Poppe amesema kwamba mchezaji wao Ramadhani Singano ‘Messi’ amehamishiwa Azam FC kinyume cha utaratibu na kila wapodai haki yao hawasikilizwi. “Mchezaji wa Yanga (Donald Ngoma) alimpiga kichwa mchezaji wetu (Hassan Kessy) na tukapeleka ushahidi wa picha za video, hakuchukuliwa hatua na wala hatukujibiwa,”. 
“Lakini Juma Nyosso (wa Mbeya City) alimdhalilisha John Bocco (wa Azam FC) akachukuliwa hatua baada ya saa 24 kwa ushahidi wa picha,”amesema.
Aidha, amesema kwamba Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), limeiamuru klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia iilipe Simba SC dola 300,000 za Kimarekani za manunuzi ya mshmbauliaji Emmanuel Okwi, lakini wanashindwa kufuatulia kwa sababu TFF haiwasikilizi tena.
“Kwa kweli tupo wakati mgumu mno, tunashindwa hata kuelewa tunacheza hii ligi kwa sababu gani, inaonekana tunawasindikiza watu ambao tayairi wameandaliwa kwa namna yoyote wawe mabingwa,”amesema.

Ni balaa Ligi Kuu Tanzania Bara

MECHI ZA LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA WIKIENDI HII
Okotba 17, 2015
Yanga SC Vs Azam FC
Majimaji FC Vs African Sports
Mbeya City Vs Simba SC
Ndanda FC Vs Toto Africans
Stand United Vs Prisons
Coastal Union Vs Mtibwa Sugar
Oktoba 18, 2015
Mgambo Shooting Vs Kagera Sugar
Mwadui FC Vs JKT Ruvu

REKODI YA SIMBA SC NA MBEYA CITY LIGI KUU

April 18, 2015
Mbeya City 2-0 Simba   
Januari 28, 2015
Simba 1-2 Mbeya City     
Februari 15, 2014
Mbeya City 1-1 Simba      
Septemba 21, 2013
Simba 2-2 Mbeya City 
MBEYA City FC leo wanaanza rasmi maisha bila kocha wao, Juma Mwambusi aliyehamia Yanga SC- watakapomenyana na wakongwe, Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mbeya City inakutana na Simba SC ikiwa na maumivu mara mbili, kwanza kumpoteza kocha wake, Mwambusi aliyekwenda kuwa Msaidizi wa Mholanzi, Hans van der Pluijm Yanga SC na pia, Nahodha wake Juma Nyosso aliyefungiwa miaka miwili.
Lakini habari njema tu ni kwamba, leo inaweza kumtumia kwa mara ya kwanza mchezaji wake mpya, Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ aliyewahi kuchezea Simba SC.
Boban amesajiliwa na Mbeya City msimu huu, lakini akachelewa kujiunga na kikosi kwa sababu ambazo hazijulikani kabla ya wiki hii kutambulishwa amejiunga na timu.
Kocha Muingereza wa Simba SC, Dylan Kerr leo akakosa huduma ya kinara wake wa mabao, Mganda Hamsi Kizza ‘Diego’ ambaye ni majeruhi, lakini Nahodha Mussa Hassan Mgosi yuko tayari kwa mchezo huo.
Msimu huu, Simba SC inaonekana kuwa vizuri kuliko Mbeya City, kwani imepoteza mechi moja tu dhidi ya mahasimu wao, Yanga SC wakati timu ya Mbeya imeshinda mechi moja tu, ikitoa sare moja na kufungwa mara nne.
Kati ya mechi hizo, moja imefungwa nyumbani na Kagera Sugar 1-0 maana yake, si ajabau hata leo wakifungwa na Simba SC nyumbani.   
Lakini ikumbukwe, Simba SC hawajawahi kuifunga Mbeya City tangu ipande Ligi Kuu, msimu wa kwanza wakitoa sare mechi zote na msimu uliopita Wekundu wa Msimbazi wakifungwa mechi zote. 
Je, leo Simba SC iko tayari kufuta uteja kwa Mbeya City? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona. 

Soka la Zanzibar sasa utulivu kurejea

Rais wa ZFA, Ravia Idarous
JITIHADA za kuurejeshea utulivu mchezo wa soka Zanzibar zimeanza kuzaa matunda baada ya klabu za Chuoni SC na Aluta SC kukubali kufuta kesi walizofungua mahakama ya mkoa Vuga dhidi ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).
Awali Chuoni ilikuwa imefungua kesi ikiilaamikia ZFA kwa kukiuka kanuni kwa kutoirudisha Ligi Kuu ya Zanzibar baada ya kushuka msimu uliopita, huku Aluta ilichukua hatua kama hiyo ikidai imenyimwa kwa njama za makusudi nafasi ya kucheza daraja la pili Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa uwanja wa Amaan jana, Katibu wa kamati hiyo Hashim Salum, alisema juzi kamati ilifanya kikao na viongozi wa timu zote mbili na kusikiliza kutoka kwao sababu za msingi zilizowafanya wafungue kesi hizo.
Hashim alisema Katibu wa Aluta Shaaban Sariboko Makarani, na meneja msaidizi wa Chuoni Bakari Hussein, wote kwa pamoja wameridhia ushauri wa kufuta kesi hizo ili kutoa nafasi mpira urejee viwanjani.
Aidha alisema, hatua hiyo pia itainufaisha klabu ya Shaba SC kurudi Ligi Kuu ya soka Zanzibar baada ya kushuka daraja pamoja na Chuoni.
Hashim alisema taratibu za kutekeleza matakwa ya kisheria ili kesi hizo ziweze kuondolewa mahakamani zilikuwa zikiendelea jana kwa kushirikisha mawakili wa wadai hao, zikitarajiwa hadi leo mchana ziwe zimekamilika.
Kwa hivyo alisema, kufuatia mafanikio hayo ya awali, kamati hiyo inaandaa utaratibu ili Ligi Kuu ya Zanzibar iweze kuanza wakati wowote kati ya Novemba 5 na 10 mwaka huu.
Katika hatua nyengine, Katibu huyo alisema wajumbe wawili wa kamati hiyo wanaondoka keshokutwa Jumatatu kwenda jijini Dar es Salaam kukutana na uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya kulijulisha mabadiliko yaliyofikiwa hadi sasa.
Wajumbe hao ni Masoud Attai na Hashim Salum mwenyewe.  

Wednesday, October 14, 2015

Arsenal yajipanga kumsajili kinda wa miaka 19


Riechedly Bazoer raia wa Holland ni moja kati ya wachezaji ambao wanaonekana kucheza vizuri sana, ukiangalia na umri wake basi ndio anazidi kuvutia wadau wa soka.
Arsenal wameshaonyesha nia ya kumsajili mchezaji huyu mwenye miaka 19 ambae kwa sasa anachezea club ya Ajax. Akiwa na miaka 16 alikataa kuhamia Arsenal ambapo Wenger alitaka kumsajili, baada ya miaka 3 ameonekana kuongeza kiwango chake na Wenger ameendeleza nia yake ya kutaka kumleta Arsenal. Kutakaa kwake kuhamia Arsenal alitaka uhakika wa kuendelea kucheza na kukua kimchezo akiwa nchini kwao Holland.
Uwezo wake na umri wake unazivutia club nyingi za Ulaya lakini Arsenal ndio inaonekana kuwa mbele kupata sign yake na kuwa Team Gunner. Endelea kufatilia shaffihdauda.co.tz ili upate habari zaidi kuhusu huyu mchezaji na Arsenal.
2D5909AD00000578-3270063-image-a-49_1444691962804

Djibril Cisse amfungulia mashitaka polisi kisi mkanda wa ngono

CRLlvGpWwAAAc1b
Cisse aliyekua mchezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa alikua na mahojiano na polisi yeye na marafiki zake watatu baada ya kuwa na kushukiwa na kesi ya kuwa na mkanda wa ngono wa mchezaji wa Olympique Lyonnais midfielder Mathieu Valbuena.
Inachosemekana ni kwamba Cisse na wenzake wamejaribu kumdai pesa mchezaji huyo ili wasiutoe mkanda huo wa ngono. Cisse alimatwa na polisi kwa ajili ya mahojiano japokua hakukua na uthibitisho kuhusu huo mkanda anao Cisse au mtu mwingine kati yao.
Bado uchunguzi upo chini ya polisi na wahusika wakuu ni Cisse na marafiki zake.

Samatta awania tuzo ya mwanasoka bora Afrika


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta kwa mara ya pili ameingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka Anayecheza Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imetoa orodha zote mbili za Mwanasoka Bora wa Mwaka Afrika na Mwanasoka Bora wa Mwaka Anayecheza Afrika.
Katika tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka Anayecheza Afrika, Samaatta mwenye umri wa miaka 23 anachezea TP Mazembe ya DRC, anachuana na Abdeladim Khadrouf wa Moghreb Tetouan ya nyumbai, Morocco, Abdelmalek Ziaya wa ES SETIF ya nyumbani, Algeria, Ahmed Akaichi wa Esperance ya nyumbani, Tunisa, Andiramahitsinoro Carolus wa Madagascar anayechezea USMA ya Algeria na Baghdad Bounedjah wa Algeria anayechezea Etoile du Sahel ya Tunisia.

Wengine ni Bakri el Madina wa El Merriekh ya nyumbani, Sudan, Bassem Morsi wa Zamalek ya nyumbani, Misri, Boris Moubhio wa AC. Leopards ya nyumbani, Kongo-Brazzaville, Djigui Diarra wa Stade Malien ya nyumbani, Mali na Felipe Ovono wa Guinea anayechezea Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Wamo pia Guelassiognon Sylvain
Gbohouo wa Ivory Coast anayecheza na Samatta T.P Mazembe, Hazem Emam wa Zamalek ya nyumbani, Misri, Hocine Ragued wa Esperance ya nyumnbani, Tunisia, Kermit Erasmus wa Orlando Pirates ya nyumbani Afrika Kusini na Malick Evouna wa Gabon, anayechezea Al Ahly ya Misri.
Wamo pia Mohamed Koffi wa Burkina Faso anayechezea Zamalek ya Misri, Mohamed Meftah wa USMA ya nyumbani, Algeria, Moudather el Tahir wa El Hilal ya nyumbani, Sudan, Oupa Manyisa wa Orlando Pirates ya nyumbani Afrika Kusini, Robert Kidiaba wa T.P Mazembe ya nyumbani, DRC, Roger Assale wa Ivory Coast anayechezea T.P Mazembe, Thamsanqa Gabuza wa Orlando Pirates ya nyumbani Afrika Kusini na 
Zein Edin Farahat wa USMA ya nyumbani, Algeria.
Katika tuzo Ya Mwanasoka Bora wa Mwaka Afrika, Yaya Toure wa Ivory Coast na Manchester City ataitetea dhidi ya Ahmed Musa wa CSKA Moscow ya Urusi na Nigeria, Andre Ayew wa Swansea City ya England na Ghana, Aymen Abdennour wa FC Valence ya Hispania na Tunisia, Baghdad Bonjah wa Etoile du Sahel ya Tunisia na Algeria.
Wengine ni Bassem Morsi wa Zamalek ya Misri, Chrisitian Atsu wa Bournemouth ya England na Ghana, Dieu Merci Mbokani wa Norwich ya England na DRC, El Arbi Hillel Soudani wa Dynamo Zagreb ya Croatia na Algeria, Faouzi Ghoulam wa Napoli ya Italia na Algeria na Ferebory Dore wa Angers ya Ufaransa na Kongo.
Yaya Toure ateteta tuzo yake ya Mwanasoka Bora wa Afrika

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Wamo pia Gervais Yao Kouassi wa Rome ya Italia na Ivory Coast, Ibrahima Traore wa Borussia Monchengladbach ya Ujerumani na Guinea, Javier Balboa wa Al-Faisaly ya Saudi Arabia na Equatorial Guinea, Heldon Ramos wa Rio Ave ya Ureno na Cape Verde, Mame Diouf wa Stoke City ya England na Senegal.
Wamo pia Max Alain Gradel wa Bournemouth ya England na Ivory Coast, Mehdi Benatia wa Bayern Munich ya Ujerumani na Morocco, Modather Al Tayeb “Karika” wa El Hilal ya Sudan, Mohamed Salah wa AS Roma ya Italia na Misri, Nicolas Nkoulou wa Marseille ya Ufaransa na Cameroon na Pierre-Emerick Aubameyang wa Borussia Dortmund ya Ujerumani na Gabon.
Wengine ni Robert Kidiaba wa T.P Mazembe, 
Rudy Gestede wa Aston Villa ya England na Benin, Riyad Mahrez wa Leicester City ya England na Algeria, Sadio Mane wa Southampton ya England na Senegal, Serge Aurier wa Paris Saint Germain ya Ufaransa na Ivory Coast na Seydou Keita wa Rome ya Italia na Mali.
Wengine ni Sofiane Feghouli wa Valencia ya Hispania na Algeria, Stephane Mbia wa Trabzonspor ya Uturuki na Cameroon, Thievy Bifouma wa Granada ya Hispania na Kongo, Victor Wanyama wa Southampton ya England na Kenya na Vincent Aboubakar wa Porto ya Ureno na Cameroon.
Wengine ni Vincent Enyeama wa Lille ya Ufaransa na Nigeria, Yacine Brahimi wa Porto ya Ureno na Algeria, Yannick Bolasie wa Crystal Palace ya England na DRC na Yasine Chikhaoui wa Al-Gharafa ya Qatar na Tunisia.