Shirika linalosimamia safari za
ndege nchini Kenya, KCAA, limetangaza kuwa anga ya Kenya itafungwa kwa
muda wa dakika hamsini siku ya Ijumaa wiki hii ili kuruhusu ndege ya
rais wa Marekani Barrack Obama kutua katika uwanja wa kimataifa wa ndege
wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi.
Kwa mujibu wa shirika hilo, agizo
hilo litatekelezwa katika viwanja vyote vya ndege nchini Kenya na kuwa
anga hiyo itafunguliwa muda tu pale ndege hiyo ya rais Obama itakapokuwa
imetua.
Shirika hilo limesema kuwa limeyaandikia mashirika yote
ya ndege na pia kampuni zote za usafiri kuhusiana na agizo hilo na kuwa
safari za ndege kadhaa zitacheleweshwa siku hiyo na pia siku ya jumapili
wakati rais Obama atakapokuwa akiondoka nchini Kenya kuelekea Ethiopia
kwa muda wa dakika arubaini.
Awali idara ya polisi nchini Kenya ilikuwa imetangaza kuwa anga yote
ya Kenya itafungwa kwa muda wa siku tatu kabla ya ziara hiyo lakini kwa
mujibu wa shirika la KCAA ndege zote zinazopaa chini ya futi elfu
ishirini hazitaruhusiwa kutua katika uwanja wa Jomo Kenyatta na uwanja
wa wilson mjini Nairobi kuanzia siku ya Ijumaa hadi siku ya jumatatu,
wakati wa kongamano la kimataifa ya ujasiriamali litakalofanyika mjini
Nairobi.
Agizo hilo sasa linamaanisha ndege zote ndogo ndogo
ambazo uhudumu kati ya Nairobi na Somalia na viwanja vingine vidogo
vidogo katika kanda ya Afrika Mashariki, havitaruhusiwa kutua Nairobi
hadi mkutano huo utakapomalizika.
Rais wa Marekani Barrack Obama
anatarajiwa mjini Nairobi siku ya Ijumaa usiku ambapo anatarajiwa kuwa
mwenyeji wa kongamano hilo la kibiashara kwa pamoja na mwenyeji wake
rais uhuru Kenyatta.
Wakati huo huo, idara ya polisi nchini Kenya imetangaza ratiba ya usafiri wakati wa mkutano huo wa kimataifa.
Barabara
kuu kati kati mwa mji mkuu wa Nairobi na zile zinazoelekea, katika
makao makuu ya umoja wa mataifa mjini Nairobi zitafungwa wakati wa
mkutano huo, na idara hiyo imetoa wito kwa Wakenya kujiepusha na
shughuli katikati mwa mji na maeneo ya mkutano huo kuanzia siku ya
ijumaa hadi siku ya jumapili.
No comments:
Post a Comment